San Salvador, El Salvador
Mashabiki 12 wa soka wamefariki dunia nchini El Salvador na wengine 90 kujeruhiwa baada ya kutokea msongamano wakati wa kuingia kwenye Uwanja wa Cuscatlan mjini San Salvador.
Tukio hilo limetoka jana Jumamosi wakati wa mechi baina ya timu za Alianza na FAS chanzo kikidaiwa kuwa ni baadhi ya mageti ya uwanja huo kufungwa na kubaki machache.
Katika kinachoaminika kuwa ni jitihada za kuingia uwanjani baadhi ya mashabiki walikosa hewa, baadhi yao wakianguka na kuzimia na wengine kufariki.
Baada ya tukio hilo, Rais Nayib Bukele alisema utaanzishwa uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo ambalo awali taarifa ya polisi ilidai kwamba watu waliofariki wanaume walikuwa saba na wanawake wawili wa umri uliozidi miaka 18 lakini taarifa ya baadaye ilitaja idadi ya waliofariki kufikia 12.
Inadaiwa kwamba baadhi ya mashabiki walikuwa wakitumia nguvu kuingia uwanjani huku pia zikiwapo taarifa kwamba wapo mashabiki waliouziwa tiketi feki za mechi hiyo.
Watu wa huduma ya kwanza walionekana wakiwasaidia waliozidiwa huku baadhi ya mashabiki wakiwa vifua wazi na kuwapepea baadhi ya majeruhi kwa kutumia mashati yao.
Na ingawa watu 90 wanadaiwa kuwa majeruhi lakini Waziri wa Afya wa El Salvador, Francisco Alabi alisema kwamba sehemu kubwa ya majeruhi waliofikishwa hospitali wako vizuri na hakuna taarifa yoyote ya kifo iliyoripotiwa hospitali.
Taarifa ya Shirikisho la Soka la El Salvador ilitangaza kuahirishwa kwa mechi zote za soka za wikiendi na kusikitishwa na kilichotokea kwenye mechi hiyo.
Kimataifa Mashabiki 12 wafariki uwanjani El Salvador
Mashabiki 12 wafariki uwanjani El Salvador
Read also
