Na mwandishi wetu
Bao pekee la Fiston Mayele, leo Jumapili limetosha kuipeleka Yanga fainali ya Kombe la FA (ASFC) na sasa inasubiri kuumana na Azam ili kumpata kinara wa michuano hiyo msimu huu wa 2022-23.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Liti, Singida, Mayele alifunga bao hilo dakika ya 82 baada piga nikupige kwenye lango la Singida na kumalizia shuti la Nkane ambalo kwanza liliokolewa na kipa Benedict Haule.
Mayele alifunga bao hilo takriban dakika mbili baada ya kocha wa Yanga, Nassredine Nabi kufanya mabadiliko akiwatoa Clement Mzize, Aziz Ki na Jesus Moloko na nafasi zao kuingia, Mayele, Tuisila Kisinda na Kennedy Musonda ambao walibadili mchezo.
Ni katika kipindi hicho hicho, Singida nao waliwatoa Francis Kazadi na Deus Kaseke na nafasi zao kuingia Meddie Kagere na Aziz Andabwile. Kaseke na Kazadi hawakufurahia mabadiliko hayo hasa Kaseke ambaye alidhihirisha hali hiyo wazi wazi.
Mabadiliko ya Nabi ndiyo kwa kiasi kikubwa yaliwapa wakati mgumu Singida ambao kwa muda mrefu walionekana kukabiliana na kasi ya Yanga, wakizuia hatari langoni mwao ingawa nao walifanya mashambulizi machache.
Katika dakika 45 za mwanzo, Yanga walionekana kufika katika lango la Singida mara kwa mara lakini umahiri wa kipa Benedict Haule ulikuwa kikwazo kwa timu hiyo kupata bao.
Mfano dakika ya 32 aliokoa vizuri shuti la mguu wa kushoto lililopigwa na Mzize, kabla ya kuokoa shuti lingine la mguu wa kushoto lililopigwa na Aziz Ki.
Katika kuiimarisha timu yake, Nabi alianza kwa kuwatoa Doumbia ambaye aliumia na Farid Mussa na kuwaingiza Nkane na Dickson Job mabadiliko ambayo hayakuisumbua sana Singida kabla ya mabadiliko ya pili yaliyozaa bao la ushindi.
Yanga ambao pia ni vinara wa Ligi Kuu NBC msimu huu, sasa wanakuwa wamefuzu fainali ya pili baada ya kufanya hivyo katika Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa Marumo Gallant ya Afrika Kusini na mambo yakiwaendea vizuri watamaliza msimu na mataji matatu au treble.
Soka Yanga yafuzu fainali FA
Yanga yafuzu fainali FA
Read also
