Na mwandishi wetu
Kesho Jumapili Yanga inashuka dimbani kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Singida Big Stars, ikieleza uwezo na ari waliyonayo itawapa faida ya kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Liti, Singida.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze ameeleza leo Jumamosi kuwa wanawaheshimu wapinzani wao kwa ubora walionao msimu huu, wakifahamu wanataka kuvuna chochote kwenye kombe hilo lakini wao wapo tayari kwa mapambano hayo.
“Tunaamini mchezo utakuwa mgumu zaidi ya ile tuliyokutana kwenye ligi, hatutaki kujificha kwenye uchovu tulionao na kutafuta sababu, lakini kiakili tunaamini tuko vizuri, tunamheshimu mpinzani ameonesha kiwango kizuri lakini tutaweka nguvu zote kuhakikisha tunaenda fainali.
“Hamasa ni kubwa sana, siyo tu ya kuchukua makombe yote lakini kuchukua tena kombe hili tulilochukua mwaka jana, tumeona furaha yake kwa mashabiki na kwetu pia. Tunajua Singida haina cha kupoteza kwa sababu hii ni mechi ya mtoano lakini tupo tayari kwa hilo,” alisema Kaze.
Naye kocha mkuu wa Singida BS, Hans Pluijm alisema wanahitaji ushindi lakini wanafahamu uzuri, ubora wa kikosi cha timu wanayokutana nayo, akifahamu mbinu zao nyingi na wao wamejifua vya kukabiliana na hilo.
“Natumaini tumejifunza makosa ya mechi ya mwisho ya nyumbani (dhidi ya Yanga) na hatutaki kuyarudia, Yanga ina kikosi imara na uwezo mkubwa na unapodhani umewakamata ndipo wanapokufunga.
“Hivyo tunahitaji umakini mkubwa kesho tunapaswa kuwa wamoja, nidhamu na kimbinu zaidi, tumejifunza mengi juu ya mechi hii, hatuwezi kueleza kila kitu jinsi tutakavyokwenda kucheza lakini tumejipanga dhidi ya Yanga,” alisema Pluijm.
Kuelekea mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 9:30 alasiri, Singida itaingia ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 4-1 na kisha 2-1 kwenye mechi mbili ilizokutana na Yanga kwenye ligi ingawa wamejinasibu kupambana kutofungwa tena.
Mshindi wa mechi hiyo, atakutana na Azam kwenye mechi ya fainali itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Azam ilitinga fainali kwa kuifunga Simba bao 2-1.
