Na mwandishi wetu
Baada ya Yanga kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha msaidizi wa timu hiyo, Cedric Kaze amesema walistahili kufika hapo ingawa bado kuna kazi wanapaswa kuimalizia katika fainali.
Yanga imetinga fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza jana baada ya kuifunga Marumo Gallants ya Afrika Kusini jumla ya mabao 4-1 na sasa itakutana na USM Alger ya Algeria iliyoifunga Asec Mimosas ya Ivory Coast mabao 2-0.
Akizungumzia namna walivyoifunga Marumo, Kaze alisema ni mbinu bora walizokuwa nazo ndizo zimewapa matokeo hayo kwani japo walikuwa wanacheza ugenini lakini walijipanga namna ya kupata mabao ya kushtukiza.
“Tulijipanga kimkakati namna ya kucheza na Marumo ugenini na haimaanishi kujipanga kujizuia tu bali tulifahamu mpinzani ukimpa upenyo wa kukushambulia, kuna sehemu atakuwa ameacha nafasi na hivyo tukafanikiwa kuzitumia na kupata ushindi.
“Ni faraja kubwa sana kuingia fainali, msimu ulikuwa mrefu na pia tumetumika sana na tunaamini tulistahili kufika hapa na pia tunafahamu kuna kazi ya fainali pia tunapaswa kuimalizia,” alisema Kaze.
Naye beki wa kati wa Yanga, Dickson Job alisema: “Ni furaha kubwa kama mchezaji mwenye ndoto sababu kwanza tumeingia hatua ya fainali, ni heshima na historia kubwa kwa nchi yote na heshima kwa sisi wachezaji.”
Job alisema kama wachezaji wako tayari kupambana kwa asilimia zote kuhakikisha wanaongeza nguvu ya kuhakikisha wanatwaa ubingwa huo pia kwa mara ya kwanza.
Fainali ya kwanza ya michuano hiyo inatarajiwa kupigwa Mei 28 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa nchini Algeria Juni 3, mwaka huu.
Endapo Yanga itafanikiwa kutwaa ndoo hiyo itaondoka na kitita cha Dola za Marekani 2,000,000 (zaidi ya Sh bilioni 4) na ikimaliza nafasi ya pili itajizolea Dola za Marekani 800,000 (zaidi ya Sh bilioni 1).
