Manchester, England
Baada ya kuichapa Real Madrid mabao 4-0 na kufuzu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya, kocha wa Man City, Pep Guardiola amewataka wachezaji wake kuanza kupiga hesabu za mataji matatu ‘treble’ msimu huu.
Siku zote Pep amekuwa akikosa ujasiri wa kuzungumzia uwezekano wa timu yake kubeba mataji matatu katika msimu mmoja lakini baada ya kuibwaga Real Madrid ameanza kupata ujasiri katika hilo.
“Kwa sasa tupo katika mbio hizo, tunaweza kufikiria hilo, tunaweza kupiga hesabu hizo, tumebakiwa na mechi tatu katika kila mashindano mechi moja, tunaweza kufanya hilo,” alisema Pep kuhusu timu yake kubeba mataji matatu.
“Ngoja kwanza nishinde mechi mbili, katika Ligi Kuu England tupo pazuri, tunajua tunahitaji mechi moja zaidi, na ningependa kusema katika fainali mbili tunacheza na jirani zetu (Man United) na nyingine na Wataliano (Inter) msimu ni mzuri, ni mzuri kweli na sasa tunatakiwa kushinda, tunajaribu kushinda hilo,” alisema Pep.
Klabu ambayo mara ya mwisho ilifanikiwa kubeba mataji matatu msimu mmoja ni Man United ambayo ilifanya hivyo mwaka 1999 wakati huo ikinolewa na Sir Alex Ferguson.
Juni 3 itaumana na Man United katika fainali ya Kombe la FA na Juni 10 itaivaa Inter Milan katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikifanikisha yote hayo ndoto ya Pep ya mataji matatu itatimia.
Ikiwa nyumbani Etihad jana Jumatano, Man City iliichapa Real Madrid mabao 4-0 na kufuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1 baada ya sare ya bao 1-1 katika mechi ya wiki iliyopita iliyopigwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu.
Man City huenda keshokutwa Jumamosi ikatangazwa kinara Ligi Kuu England (EPL) iwapo Arsenal itapoteza mechi Jumamosi vinginevyo itabidi isubiri ishinde mechi yake ya Jumapili ili ilibebe taji hilo la msimu 2022-23.
Man City jana ilineemeka na mabao ya Bernardo Silva aliyefunga mawili katika dakika za 23 na 37 wakati mengine mawili yalifungwa na Akanji dakika ya 76 na Alvarez aliyefunga la nne dakika ya 90.
