Na mwandishi wetu
Yanga kesho Jumamosi wanatarajia kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu NBC kama watafanikiwa kuifunga Dodoma Jiji katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Iwapo Yanga itashinda mechi hiyo itafikisha pointi 74 na kuutetea ubingwa ikiwa na mechi mbili mkononi, mtani wao, Simba anayeshika nafasi ya pili kwa pointi 64 au timu nyingine hazitoweza kufikia pointi hizo.
Simba yenye pointi 64 ambayo leo Ijumaa jioni inatarajia kukipiga na Ruvu Shooting hata kama ikishinda michezo mitatu iliyobaki kufunga pazia la ligi msimu huu itafikisha pointi 73.
Yanga inarejea kuivaa Dodoma ikiwa imetoka kuichapa Marumo Gallants ya Afrika Kusini mabao 2-0 katika nusu fainali ya mchezo wa mkondo wa kwanza kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Hali ipo tofauti kwa Dodoma ambao wako nafasi ya 10 wakiwa na pointi 31, wanahitaji ushindi na wakipoteza watajiweka kwenye presha ya kushuka nafasi za chini zaidi kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema mechi hiyo itakuwa ngumu kwani wachezaji wamechoka na wengine ni majeruhi hivyo wale wasiopata nafasi mechi iliyopita ya Kombe la Shirikisho watatumika.
Mshambuliaji Fiston Mayele alisema haitakuwa mechi nyepesi lakini wanajua umuhimu wa mechi hiyo kwa sababu anaamini wakipata pointi tatu tayari watakuwa mabingwa kwa hiyo hawawezi kuacha hiyo nafasi ipite.
Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope alisema: “Tunajua Yanga ni timu kubwa na nzuri na imecheza kwa muda mrefu lakini tutatumia mapungufu yao madogo waliyonayo ili tupate ushindi.”
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo, Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mchezo mwingine utakaochezwa kesho wa ligi hiyo ni kati ya Geita Gold na Mbeya City utakaochezwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita.
Soka Yanga kutangaza ubingwa?
Yanga kutangaza ubingwa?
Read also
