Na mwandishi wetu
Bondia wa ngumi za kulipwa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Seleman Kidunda leo Alhamisi ameingia mkataba wa pambano dhidi ya Eric Mukadi raia wa DR Congo.
Pambano hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Ngumi za Kulipwa ya PFA Promotion Entertainment linatarajiwa kupigwa Juni 30, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Pia pambano jingine siku hiyo linatarajiwa kuwa baina ya Mfaume Mfaume atakayezichapa na Nkululeko Mhlongo raia wa Afrika Kusini.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi la kusaini mikataba kwa mabondia hao, Mkurugenzi wa PFA, Fadhili Maogola alisema wameamua kumchukua Kidunda kutokana na kutambua ubora wake wakiamini atatoa upinzani wa kutosha kwa mpinzani wake huyo.
“Tumempa mkataba Kidunda kwa ajili ya pambano letu la Hata Usipolala Patakucha Tu, yeye na Mfaume watapanda katika ulingo mmoja siku hiyo pale Mlimani City kuonesha ukali wao katika mapambano haya ya kimataifa maana hakuna asiyejua ubora wao,” alisema Maogola.
“Lakini mbali na hao pia wapo wakali wengine ambao watapanda ulingoni kuonesha ufundi wa mchezo wa ngumi, rai yetu ni kwamba tunawaomba wadhamini wajitokeze kwa wingi kuhakikisha tunalipa hadhi pambano letu,” alisema Maogola.
Kwa upande wake Kidunda alisema: “Nashukuru kwa kupata hili pambano kwa sababu mara ya mwisho nilipanda ulingoni kule Songea katika pambano langu la Katompa, mashabiki wangu nataka kuwaambia narudi tena kwa moto mkubwa maana siku zote mimi sipigani ila nacheza ngumi.”
