Na mwandishi wetu
Jumamosi hii, mahasimu wa jadi, Simba na Yaanga wanatoana jasho. Siku
kadhaa kabla ya mechi hii, mashabiki hucharurana kwa majigambo na
ahadi mbalimbali na mwisho wa mechi wako wanaotoka vichwa chini na
wengine wakiwa na furaha.
Katika miaka ya karibuni mashabiki wameingia katika matukio au
utamaduni mpya wa kuzimia uwanjani mara inapotokea timu yao kufungwa
wakati mechi ikiendelea, matukio ambayo huko nyuma hayakuwa ya kawaida
au hayakuwahi kuripotiwa.
Mechi ya mwaka 2014 ya Nani Mtani Jembe ambayo Yanga ililala kwa mabao
2-0 wakati huo ikinolewa na Mbrazil Marcio Maximo na Simba ikinolewa
na Mzambia Patrick Phiri, inaweza kuwa mfano mzuri wa matukio ya
mashabiki wengi kuzimia.
Wakati wikiendi hii timu hizi zikiumana, si vibaya kujiuliza ni kwa
nini mashabiki kwa miaka ya karibuni wamekuwa wakianguka na kuzimia
majukwaani wakati mechi ikiendelea, na kwa nini hali hiyo haikuwapo
miaka ya nyuma au haikuwa kubwa miaka ya nyumba.
Je ni kweli kwamba mapenzi ya soka katika klabu hizi yamekuwa makubwa
sana kwa miaka ya karibuni kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma? Kwamba
hiyo ndiyo sababu kubwa ya mashabiki kuzimia uwanjani wakati mechi
ikiendelea?.
Je ni kweli kwamba mashabiki wa sasa hawana uvumilivu, hamasa yao iko
juu kwamba soka kwao ni burudani ya kuwapa matokeo mazuri tu na si
vinginevyo na hivyo inapotokea timu yao kushindwa huona kama
wameumizwa kiasi kikubwa na hivyo kuishiwa nguvu na hatimaye kuzimia?
Vipi kuhusu madai kwamba kizazi cha sasa si sawa na cha zamani katika
mambo ya lishe, yaani chakula kinacholiwa sasa si cha asili,
kinawasababishia madhara watu wengi wakiwamo mashabiki wa soka ambao
wakiumizwa kidogo tu moyo hushindwa kuhimili na hivyo kujikuta
wakianguka na kuzimia.
Na vipi kuhusu mfumo wa maisha kwamba maisha ya sasa ni tofauti na
yale ya zamani ya watu kufanya kazi za kuushughulisha mwili, kutembea
umbali mrefu bila usafiri hali ambayo ni tofauti na maisha ya sasa
ambayo yanadaiwa kuwafanya watu kuwa legelege, wavivu ambao hushindwa
kukabiliana na matukio ya kuumizwa moyo, misukosuko kidogo tu mtu
anajikuta akizimia.
Mtaalam wa saikolojia jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa
jina anasema tatizo mojawapo linaweza kuwa ni matumaini makubwa
anayokuwa nayo shabiki.
“Mtu anaingia uwanjani akiwa tayari amewatambia wenzake akiamini
anatoka na ushindi na wengine hadi kutoa ahadi za ajabu ajabu, sasa
mtu wa aina hii anaposhindwa sishangai kusikia amezimia,” anasema.
Akifafanua kuhusu ahadi anasema kuna wanaowekeana pesa tena nyingi,
sasa mtu wa aina hii anaposhindwa anakuwa katika mazingira magumu,
anaifikiria pesa yake na hasara anayoipata na hiyo inaweza kuwa sababu
mojawapo ya mtu huyo kuzimia.
Anaongeza kuwa wapo mashabiki ambao huenda uwanjani na matokeo kabla
hata mechi haijachezwa na matokeo yanapokuwa tofauti anajikuta akiwa
mnyonge na hapo ndipo nguvu zinamuishia na kujikuta akizimia au kuwa
mnyonge isivyo kawaida.
Akizungumzia suluhisho la tatizo, anasema kwamba kwanza shabiki yeyote
anatakiwa kufahamu kwamba mpira ni burudani hivyo aingie uwanjani
akiamini atashinda lakini atambue kwamba kushindwa pia kupo.
Anaongeza kuwa mashabiki waache tabia ya kujiwekea malengo makubwa
kwenye mechi kwani wao si wanaocheza, “fulani leo lazima atoke
uwanjani na bao, kauli za aina hii ni za kujiamini mno lakini kibaya
zaidi ni kwamba unajiaminisha kupitia mtu mwingine ambaye huna uhakika
kama naye ana malengo kama hayo, mwengine atasema Mayele, mwengine
atamtaja Bocco, hili si jambo zuri.
“Kweli hawa ni washambuliaji wazuri na wana uwezo mkubwa wa kufunga na
kila shabiki ana haki ya kujivunia mchezaji wake lakini pia tambua
kwamba wanakutana na mabeki wazuri wenye uwezo wa kuzuia hivyo si
sahihi kuamini kwamba ni lazima watoke uwanjani na bao,” anasema.
Anashauri mashabiki kuwa na tabia ya kujipa matumaini na si kuweka
malengo huku wakijiamini hadi kufikia hatua ya kuwekeana ahadi ya
kutoa pesa au mke au nyumba, shabiki wa aina hii anapofungwa
akifikiria ahadi aliyoitoa anaishiwa nguvu na si ajabu kuzimia.
“Ni kweli kwamba ushindi ni mtamu na kila shabiki anaiamini timu yake
itashinda, hilo si jambo baya lakini imani hiyo isipitilize, matumaini
yawe ya kawaida, malengo yawe ya kawaida, weka akiba kwamba kushindwa
pia kupo.
“Jipe imani ya ushindi kwani ushindi ni mtamu lakini pia si vibaya
kujiandaa kukabiliana na kushindwa na kuikubali hali hiyo, ukifanya
hivyo hutoumia sana unaposhindwa na kama ni kuwekeana ahadi utaweka za
kawaida tu ambazo unazimudu, hutoweka ahadi za ajabu ajabu za kumtoa
mke wako, nyumba yako au pesa nyingi,” anasema.
Maswali yanaweza kuwa mengi kuhusu huu utamaduni wa kuzimia, mwingine
anaweza kwenda mbali na kujiuliza, vipi kuhusu mabadiliko ya tabia
nchi? Kwamba siku hizi mazingira yameharibiwa kiasi kwamba hewa chafu
imekuwa ikiathiri watu, je hili nalo linaweza kuchangia mashabiki
kuzimia uwanjani wakati timu zao zikiumana baada ya kuumizwa na
matokeo mabaya?
Vipi kuhusu kucharurana na majigambo? Je nayo hayana nafasi katika
kuwakatisha tamaa mashabiki baada ya timu zao kushindwa na kuona
kwamba watakuwa na wakati mgumu mitaani na vijiweni kwamba zamani
mashabiki hawakuwa wakicharurana katika namna inayoumiza vibaya na
hivyo shabiki wa sasa anapolifikiria hilo anaumia, anakata tamaa na
kujikuta akianguka na kuzimia.
Tunaweza kuwa na hoja nyingi lakini matukio haya au utamaduni huu mpya
katika soka nchini unaacha maswali mengi kwamba kulikoni yamekuwa
yakitokea miaka ya karibuni wakati miaka ya nyuma hali haikuwa hivyo.
Vipi ongezeko la idadi ya watu nalo limechangia?
Soka Kulikoni mashabiki Simba, Yanga kuzimia uwanjani!
Kulikoni mashabiki Simba, Yanga kuzimia uwanjani!
Read also
