London, England
Klabu za Tottenham Hotspur na Crystal Palace zinashirikiana na polisi wa London kumsaka shabiki anayedaiwa kumtolea dhihaka za kibaguzi mshambuliaji wa Spurs, Son Heung-Min.
Son ambaye ni raia wa Korea Kusini alikumbana na kadhia hiyo Jumamosi iliyopita wakati akitoka uwanjani katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) iliyozikutanisha Spurs na Palace.
Video za kwenye mitandao ya kijamii zimemuonyesha shabiki mmoja anayeaminika kuwa ni wa Spurs akimtolea ishara za ubaguzi wa rangi mchezaji huyo wakati akipita mbele ya mashabiki wa timu hiyo katika mechi ya EPL ambayo Spurs ilishinda kwa bao 1-0.
“Tunafahamu uwapo wa video ambayo imeonekana kwenye mitandao ikimuonesha shabiki kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur akitoa ishara za ubaguzi wa rangi kwa mshambuliaji huyo wa Korea Kusini wakati akitoka uwanjani baada ya kufanyiwa mabadiliko,” ilieleza Palace katika taarifa.
“Ushahidi umewasilishwa polisi na atakapobainika atakumbana na adhabu ya kufungiwa na klabu, hatuwezi kuvumilia tabia za aina hii katika klabu yetu,” ilifafanua taarifa hiyo.
Mwaka jana klabu ya Chelsea ilitangaza kumfungia shabiki wake mwenye tiketi ya msimu kuhudhuria mechi baada ya kuwapo taarifa za Son kufanyiwa dhihaka za kibaguzi katika mechi ya EPL iliyopigwa kwenye dimba la Stamford Bridge.
Spurs nayo iliahidi kutoa ushirikiano katika kadhia hiyo ili mhusika aadhibiwe, “Tutafanya kila liwezekanalo kwa nguvu zetu kuhakikisha mhusika anakamatwa hatua kali zinachukuliwa kama ilivyokuwa msimu uliopita, Son alipofanyiwa dhihaka hizo katika mechi na Chelsea.”
