Na mwandishi wetu
Prince Dube ameendelea kuinyanyasa Simba baada ya leo Jumapili kufunga bao la ushindi lililoiwezesha Azam kuilaza Simba mabao 2-1 na kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (FA) kwa ushindi wa mabao 2-1.
Hilo ni bao la tatu kwa Dube kuifunga Simba akiwa tayari ameshainyanyasa timu hiyo mara mbili lakini ushindi wa leo umekuwa na maana kubwa kwa timu yake ambayo imepania kubeba taji la michuano hiyo msimu huu.
Kwa ushindi huo uliopatikana kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Azam sasa inasubiri kwenda kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga kucheza mechi ya fainali dhidi ya mshindi wa mechi ya Yanga na Singida Big Stars.
Azam ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 22 mfungaji akiwa Lusajo Mwaikenda aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Ayoub Lyanga na kuokolewa na kipa wa Simba, Ally Salim.
Simba hata hivyo walipambana na dakika sita baadaye walifanikiwa kusawazisha bao hilo mfungaji akiwa ni Sadio Kanoute na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Mambo yalikwenda kombo kwa Simba katika dakka ya 75 baada ya Dube aliyetokea benchi kuinasa pasi ya kichwa akiwa upande wa kushoto wa Simba na kupiga mpira wa juu uliokwenda moja kwa moja wavuni.
Beki wa Simba, Henock Inonga alijaribu kuuwahi mpira huo huku mshambuliaji wa Azam, Abdul Sopu naye akiwa karibu kabisa na lango ili kumalizia kazi ya Dube kama kungekuwa na ulazima wa kufanya hivyo lakini si Inonga wala Sopu aliyeugusa mpira huo wa juu ambao ulijaa wavuni.
Simba ilipambana ikiwania kusawazisha bao hilo kabla ya kumuingiza mshambuliaji wake mkongwe John Bocco ambaye alifanikiwa kupiga shuti moja kali la mguu wa kushoto ambalo kama si umahiri wa kipa wa Azam Idris Abdoulah mambo yangekuwa mengine.
Simba pia ilipata pigo baada ya Kanoute kulimwa kadi ya pili ya njano na kutoka uwanjani kwa kucheza rafu na hivyo timu hiyo kubaki na wachezaji 10 uwanjani.
Akizungumzia matokeo hayo, kocha msaidizi Simba, Juma Mgunda alisema kwanza wameyakubali lakini pia yamewaamsha na kuwapa nafasi ya kujitathmini ili kuangalia marekebisho ya kufanya katika timu yao.
Naye kocha msaidizi Azam, Kally Ongalla aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kupata ushindi huku akisisitiza kwamba bado wana kazi ya kufanya kwani wanalitaka kombe la michuano hiyo ambayo mshindi wake hujikatia moja kwa moja tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Soka Azam yatua fainali FA, yaibwaga Simba
Azam yatua fainali FA, yaibwaga Simba
Read also
