Na mwandishi wetu
Timu ya Ruvu Shooting imeeleza kuwa kulingana na wapinzani wanaotarajia kukutana nao kwenye mechi tatu zilizobaki za Ligi Kuu NBC, hawana pa kuegemea zaidi ya kumwachia Mungu awatetee.
Ruvu inayopambana isishuke daraja msimu huu, inaburuza mkia kwa pointi zao 20 baada ya kucheza mechi 27.
Ofisa Habari wa Ruvu, Masau Bwire amesema katika mechi hizo wataanza na Simba kisha Singida Big Stars na mwisho Dodoma Jiji akiamini hizo zote ni mechi ngumu kwao.
Bwire alisema kwamba pamoja na maandalizi waliyonayo lakini wanamtanguliza Mungu kuwaepusha na kikombe cha kushuka daraja kupitia mechi hizo.
“Mechi iliyo mbele yetu tunayoitazama ni ya Simba, kwa hali tuliyonayo, nafasi tuliyopo na uwezo tulionao kisoka, kikubwa zaidi kwa sasa ni kumtanguliza Mungu kwa maana ya maombi zaidi.
“Simba tumewaona kwenye mashindano ya mabingwa, pamoja na kuondolewa lakini ubora wao tumeuona, ni moja ya timu bora Afrika kwa sasa kwa hiyo ni mechi ngumu kwetu na ndio nikasema pamoja na maandalizi tuliyonayo lakini tumekuwa kama na wasiwasi kutokana na hali zetu hivyo Mungu pekee anaweza kutusaidia kwa sasa, tuongeze maombi,” alisema Bwire.
Ofisa huyo alifafanua kuwa anafahamu Watanzania wengi wanavutiwa na soka la Ruvu hivyo ni heri wakawasaidia katika maombi hayo ili wapate matokeo katika mechi hizo na mwisho wasalie ligi kuu msimu ujao.
