Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema siri ya ushindi wao dhidi ya Singida Big Stars ni wachezaji kucheza kwa kujitoa bila kujali uchovu waliokuwa nao kwa kucheza mechi mfululizo.
Yanga juzi Jumatano ilikuwa ugenini Uwanja wa Liti, Singida na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida Big Stars matokeo ambayo yamewafanya kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC na sasa wanahitaji pointi tatu ili kutetea ubingwa ligi hiyo.
Kaze ameeleza kuwa mbali na wachezaji wao kucheza kwa kujituma lakini mbinu waliyotumia ya kupeleka mashambulizi ya kasi kwenye lango la wapinzani wao, imesaidia kumaliza mchezo huo mapema.
“Lengo letu lilikuwa ni kupata mabao ya haraka na mbinu tuliyoingia nayo ni kupiga mipira kwenye nafasi na wachezaji wetu wa pembeni kukimbia, hicho kiliwachanganya Singida na kufanikiwa kupata mabao hayo ambayo kwetu ni furaha sababu tumetimiza lengo,” alisema Kaze.
Kocha Mkuu wa Singida BS, Hans Pluijm kwa upande wake amekiri kuwa kipigo hicho kimetokana na kuzidiwa kimbinu na wapinzani wao, kitu ambacho kilisababisha waruhusu mabao mawili ya haraka.
“Hatukucheza kwenye kiwango kile ambacho tulitarajia, hata tulivyorudi kipindi cha pili tulijaribu kupambana kutafuta mabao ya kusawazisha lakini bado hatukuweza kucheza kwenye kiwango kile ambacho tulikitarajia,” alisema Pluijm.
Pluijm alisema wanayakubali matokeo hayo na wanarudi kujpanga ili kuhakikisha wanalipa kisasi kwa kushinda mchezo wa nusu fainali wa michuano ya Kombe la FA (ASFC) dhidi ya Yanga ambao utachezwa kwenye uwanja huo huo wa Liti.
