Na mwandishi wetu
Yanga sasa imebakisha mechi moja tu kabla ya kutawazwa vinara wa Ligi Kuu NBC msimu wa 2022-23 baada ya kuichapa Singida Big Stars mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa Alhamisi hii jioni kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha pointi 71 na iwapo itashinda mechi ijayo na Dodoma Jiji itafikisha pointi 74 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote inayoshiriki ligi hiyo na hivyo kulibeba taji la ligi kwa mara ya pili mfululizo
Katika mechi na Singida Big, Yanga ilineemeka na mabao ya kipindi cha kwanza yaliyofungwa na Stephane Aziz Ki dakika ya 15 na Clement Mzize aliyefunga la pili katika dakika ya 20.
Aziz Ki kama kawaida yake alifunga bao hilo kwa shuti kali akidhihirisha kwa mara nyingine uwezo wake wa kufumua mashuti yenye tija wakati Mzize alifunga bao lake akiitumia pasi ya Jesus Moloko.
Matokeo hayo yanaiweka pagumu Simba katika dhamira yake ya kuishusha Yanga kileleni hasa baada ya timu hiyo kukubali sare ya bao 1-1 mbele ya Namungo Jumatano hii wakati ikiwa ugenini Lindi kwenye Uwanja wa Majaliwa.
Simba sasa imezidiwa na Yanga kwa tofauti ya pointi saba ingawa lolote linaweza kutokea katika mechi tatu zilizobaki kabla ya pazia za ligi msimu huu kufungwa rasmi.
Kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda akizungumzia nafasi yao katika kulibeba taji la Ligi Kuu NBC, alinukuliwa na GreenSports akisema kwamba hawajakata tamaa katika mbio za ubingwa hadi mwisho utakapofika.
“Haiwi mwisho mpaka ifike mwisho, tutarudi kujirekebisha kuendelea na mapambano katika michezo iliyobaki kujua hatma yetu ya ubingwa,” alisema Mgunda mara baada ya sare ya bao 1-1 na Namungo.
