New York, Marekani
Cristiano Ronaldo ndiye mwanamichezo anayelipwa fedha nyingi zaidi duniani kwa sasa akiwabwaga wanasoka wenzake, Lionel Messi na Kylian Mbappe wa PSG.
Kwa mujibu wa taarifa za mwaka 2023 za jarida maarufu duniani la mambo ya uchumi la Forbes, Ronaldo ameshika namba moja tangu ajiunge na klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia na mshahara wake kuongezea karibu mara mbili ya aliokuwa akiupata awali.
Ronaldo alichukua uamuzi wa kuihama Man United mwaka jana na kujiunga na klabu hiyo ya Saudi Arabia huku akiwashutumu wamiliki wa klabu yake ya zamani, baadhi ya wachezaji na kocha wake.
Kwa sasa mchezaji huyo ana mkataba na klabu ya Al Nassr ambao unafikia ukomo mwaka 2025 na kwa mujibu wa Forbes pato lake lilifikia dola 136 milioni huku mshahara wake wa mwaka ukidaiwa kuongezeka na unakadiriwa kufikia dola 75 milioni.
Baadhi ya vyombo vya habari vilidai kwamba mkataba wake na klabu hiyo ya Saudi Arabia una thamani ya Dola 219.98 milioni.
Kwa mujibu wa Forbes, Messi anashika nafasi ya pili akiwa na pato linalofikia Dola 130 milioni wakati nafasi ya tatu inashikiliwa na Mbappe ambaye pato lake linafikia Dola 120 milioni.
Nafasi ya nne inashikiliwa na nyota wa mpira wa kikapu, LeBron James ambaye pato lake linafikia Dola 119.5 milioni huku bondia wa Mexico, Canelo Alvarez akifunga idadi ya tano bora kwa pato linalofikia Dola 110 milioni.
Orodha kamili ya wanamichezo 10 wanaolipwa fedha nyingi zaidi duniani ni kiasi cha fedha wanachopata ni kama ifuatavyo…
- Cristiano Ronaldo (Dola 136 milioni)
- Lionel Messi (Dola 130 milioni)
- Kylian Mbappe (Dola 120 milioni)
- Lebron James (Dola 119.5 milioni)
- Canelo Alvarez (Dola 110 milioni)
- Dustin Johnson (Dola 107 milioni)
- Phil Mickelson (Dola 106 milioni)
- Stephan Curry (Dola 100.4 milioni)
- Roger Federer (Dola 95.1 milioni)
- Kevin Durant (Dola 89.1 milioni)
