Na mwandishi wetu
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza kuziongezea fedha timu za Simba na Yanga kufikia Sh milioni 10 kwa kila bao watakalofunga endapo zitavuka kucheza hatua ya nusu fainali za michuano ya klabu Afrika.
Tamko hilo limetolewa leo Ijumaa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akieleza kuwa ahadi hiyo imekwenda sambamba na ujumbe wa Rais Samia akizitaka timu hizo kutumia maarifa yao yote kuhakikisha zinatinga nusu fainali.
Ahadi hiyo ni ongezeko la asilimia 100 kutoka ile ya awali ambapo kila bao walilokuwa wakifunga walikuwa wanazawadiwa Sh 5,000,000 mpaka kufikia hatua waliyopo sasa ya robo fainali.
“Pamoja na ahadi hiyo mheshimiwa Rais Samia anazitakia kila la heri Simba na Yanga na amewataka wachezaji kujituma uwanjani na kutumia maarifa yao yote kuhakikisha wanashinda michezo ya kukamilisha robo fainali ili wafanikiwe kuingia nusu fainali ambapo kila goli litakuwa Shilingi milioni 10,” alisema Msigwa.
Katika ufafanuzi wake, Msigwa aliongeza kuwa fedha itakayotolewa juu ya mabao hayo ya nusu fainali ni kwa mabao yatakayofungwa ndani ya dakika 90 au 120 za mchezo na si mabao ya mikwaju ya penalti baada ya kumalizika kwa mchezo.
Simba leo saa 4.00 usiku itakuwa ugenini kupepetana na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Wydad AC ya Morocco kwenye Uwanja wa Mohamed V, Casablanca.
Kwenye mechi ya awali iliyopigwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Simba iliwafunga wapinzani wao hao bao 1-0 na hivyo inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote kupenya nusu fainali.
Yanga ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ilishinda mabao 2-0 ugenini dhidi ya Rivers United ya Nigeria na Jumapili hii itarudiana na timu hiyo kwenye Uwanja wa Mkapa.
Kwenye ahadi ya awali, Simba imefunga mabao 11 kama ilivyofanya Yanga na kila moja kuchota Sh milioni 55 kuanzia mabao ya mechi za makundi mpaka mechi za mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali.
Kimataifa Rais Samia anunua bao kwa milioni 10
Rais Samia anunua bao kwa milioni 10
Read also
