Barcelona, Hispania
Kocha wa Barca, Xavi Hernandez amesema ataendelea kulalamikia tatizo la viwanja kukosa ubora katika mechi za La Liga licha ya kudhihakiwa.
Katika malalamiko yake Xavi anataka iwepo sheria ya kusimamia ubora wa viwanja kwenye eneo la kuchezea ikiwa ni siku chache baada ya kulalamikia ubovu wa uwanja katika mechi yao na Getafe.
Barca ilibanwa na kulazimishwa sare ya 0-0 na Getafe wiki iliyopita kwenye dimba la Coliseum Alfonso lakini Xavi alidhihakiwa alipolalamika akidai kutoridhishwa na ubora wa uwanja huo.
Baada ya mechi hiyo, Xavi alalamika akisema kuhusu uwanja kuwa mkavu na wenye nyasi ndefu akidai kwamba uwanja wa aina hiyo hauwasaidii hasa mnapocheza mchana wa jua.
Xavi mara kwa mara amekuwa akilalamikia viwanja kwenye maeneo ya kuchezea ambavyo amedai si vizuri hasa mnapocheza kwa kupasiana na kusisitiza kuwa ataendelea kulalamika bila kujali anadhihakiwa kiasi gani.
“Nakosolewa kwa kila kitu, hilo halinikeri, sijali ni kwa kiasi gani nadhihakiwa lakini siwezi kukaa kimya, viwanja vikavu havitusaidii,” alisema Xavi.
“Hili ni swali kwa Sanchez Flores (kocha wa Getafe) kwa nini viwanja havimwagiwi maji, na kwa nini majani ni marefu isivyo kawaida,” alihoji Xavi.
“Sitanyamaza hadi kuwe na sheria ya ubora wa eneo la kuchezea, ipo sheria hiyo kwenye michezo mingine, kwenye golfu majani yakiwa marefu wanayakata, kwenye tenisi kama mvua inanyesha wanasimamisha mechi,” alisema Xavi.
Sare ya Barca kwa Getafe ni mechi ya pili mfululizo kwa timu hiyo kwenye La Liga isiyo na matokeo mazuri lakini ni mechi ya tatu mfululizo bila ushindi katika michuano yote lakini Xavi anasema kwamba kwake matokeo si kitu muhimu.
“Tungeweza kutoka sare kwenye uwanja ulio bora, hapa si suala la jinsi mechi ilivyoisha kwani huwa nasema kuhusu tatizo la uwanja hata pale tunaposhinda mechi,” aliongeza.
Barca hata hivyo inaendelea kushika usukani kwenye La Liga ikiongoza kwa tofauti ya pointi 11 zikiwa zimebaki mechi tisa kabla ya ligi hiyo kufikia tamati na leo Jumapili timu hiyo itakuwa nyumbani Nou Camp kuumana na Atletico mechi ambayo Xavi amewataka wachezaji wake kurudi katika ubora wao.
