Na mwandishi wetu
Simba, leo Jumamosi imewapa mashabiki wake zawadi ya Eid el Fitr baada ya kuichapa Wydad Casablanca bao 1-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Simba ilipata bao hilo katika dakika ya 31 mfungaji akiwa ni Jean Baleke, bao ambalo lilianzia kwa mpira wa adhabu uliopigwa na Saido Ntibazonkiza kabla ya kuokolewa na kumkuta Kibu Dennis.
Kibu naye akafumua shuti kali ambalo, Baleke akiwa amejiweka katika eneo zuri akamalizia kwa kuujaza mpira wavuni na kuwaamsha vitini mashabiki wa Simba waliofurika uwanjani hapo.
Baada ya bao hilo Simba haikucheza kwa kulinda ushindi wao badala yake iliendelea kuisakama Wydad ambapo dakika ya 35 ilifanya mashambulizi yaliyotengeneza kona mbili ambazo hazikuzaa matunda.
Simba iliendelea na kasi hiyo katika kipindi cha pili, sekunde chache baada ya kuanza kipindi hicho, Clatous Chama aliufumania mpira karibu na eneo la 18 na kufumua shuti ambalo halikuzaa matunda.
Shomari Kapombe naye katika dakika ya 68 akiwa amepanda mbele upande wa kulia alifumua shuti la chinichini lililotoka sentimita chache nje ya lango la Wydad.

Wydad nao walijibu mapigo katika dakika ya 72 baada ya Al Mutaraj kuambaa na mpira upande wa kushoto karibu na lango la Simba lakini wakati akitaka kumpiga chenga Henock Inonga beki huyo alikuwa makini na kufanikiwa kuutoa mpira nje na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kibu alijibu shambulizi hilo la Wydad dakika dakika mbili baadaye, akiwa upande wa kushoto aliunasa mpira na kufumua shuti la juu ambalo lilionekana kuelekea kwenye upande wa kushoto wa goli la Wydad lakini mpira huo ulitoka nje kidogo la lango.
Katika hali ambayo iliwashangaza mashabiki, Hamid Ahadad alionekana kuzidiwa ujanja na Kibu na kuamua kumvuta shati waziwazi wakati Kibu akimlamba chenga na mchezaji huyo wa Wydad kulimwa kadi ya njano hapo hapo.
Dakika tatu kabla ya mpira kumalizika Wydad walifanya shambulizi langoni mwa Simba baada ya Al Mutaraj kufumua shuti lakini Joash Onyango aliokoa mpira huo na kuwa kona ambayo kipa wa Simba Ali Salim aliuwahi mpira ukiwa juu na kuondosha hatari langoni mwake.
Zikiwa zimebaki kama dakika tano mpira kumalizika kocha wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ alimuingiza John Bocco kuchukua nafasi ya Baleke.
Matokeo ya mechi ya leo ambayo ilichezwa huku kukiwa na mvua za hapa na pale yanaifanya Simba kuwa pa kuanzia kwani sasa itaingia uwanjani kucheza mechi ya marudiano ugenini kusaka tiketi ya nusu fainali ikiwa na mtaji wa bao hilo pekee.
