Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele amesema kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin alimpigia simu kumuomba radhi baada ya kukwazana katika mchezo wa watani wa jadi uliochezwa Jumapili iliyopita.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Mayele alilalamika kutendewa madhambi na Mzamiru wakiwa wanawania mpira hadi kumlazimu mchezaji huyo kutolewa nje kwa ajili ya matibabu.
Mayele alisema mchezaji huyo wa Simba alimpigia simu kumuomba radhi na kumwambia kuwa hakukusudia kufanya kosa ila ilitokea bahati mbaya.
“Mzamiru alinipigia simu nikaongea naye, akaniambia kilichotokea uwanjani ni bahati mbaya hakufanya kwa makusudi, ukweli niliumia kidogo lakini nashukuru nilipata muda wa kupumzika na jana nilianza mazoezi,” alisema Mayele.
Mayele baada ya kuumizwa alionekana kuhamaki kiasi cha kutaka kuanzisha ugomvi lakini wachezaji wenzake na wengine wa Simba walimzuia kufanya hivyo. Katika mchezo huo Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-0.
Mshambuliaji huyo wa Yanga alitoka kwenye mchezo huo akiwa anachechemea lakini ameungana na timu kuelekea Nigeria kwa ajili ya mchezo wa robo fainali wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa Jumapili hii.
