Na mwandishi wetu
Yanga inaelekea Nigeria kuvaana na Rivers United kwenye mchezo wa robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa kamili isipokuwa kipa Aboutwalib Mshery (pichani) ambaye ni majeruhi wa muda mrefu.
Kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka kesho Alfajiri na ndege ya Shirika la Ethiopia kwa ajili ya mchezo wao huo wa mkondo wa kwanza utakaopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa wa Godswill, Akwa Ibom.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema wakiwa Addis Ababa wataungana na beki wao wa kati, Mamadou Doumbia aliyekuwa Mali kwa ajili ya msiba wa baba yake mzazi na sasa ameshamaliza shughuli za mazishi.
“Wachezaji wote wako kwenye hali nzuri na hatuna majeruhi kasoro Mshery mwenye majeraha ya muda mrefu, Mamadou ambaye alipata msiba wa baba yake mzazi amemaliza salama shughuli zote za mazishi na tutakutana naye Addis Ababa, Ethiopia na kwenda naye pamoja nchini Nigeria.
“Tunakwenda kucheza mchezo mkubwa na muhimu kwenye historia ya klabu yetu ugenini, tunawaomba wanachama, mashabiki na wapenzi wa Yanga kuiombea klabu yetu iweze kufanya vizuri kwenye mchezo huu muhimu wa kwanza wa robo fainali,” alisema Kamwe.
Ofisa huyo pia alisema kwamba tiketi za mechi ya marudiano dhidi ya Rivers mchezo unaotarajiwa kupigwa Aprili 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, zimeanza kuuzwa jana.
Alisema kwa wadhifa alionao katika klabu hiyo, anajivunia kuona mashabiki na wapenzi wa Yanga wanabadili utamaduni na kununua tiketi mapema, kwani hiyo inaongeza morali kubwa kwa wachezaji kuelekea maandalizi ya mchezo wa marudiano.
Yanga inakwenda Nigeria ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Rivers ugenini na kisha nyumbani kwa idadi hiyo hiyo kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na kutupwa nje ya michuano hiyo.
