Na mwandishi wetu
Aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya KMC, Thierry Hitimana amesema hataki kuzungumzia kwa kina kuhusu kufutwa kazi na timu hiyo lakini anaamini anastahili kubeba lawama zote.
Hitimana raia wa Rwanda ameyasema hayo leo Jumamosi ikiwa ni siku mbili zimepita tangu uongozi wa KMC ulipotangaza kuvunja mkataba na kocha huyo kutokana na kutoridhishwa na matokeo mabovu ya timu msimu huu.
Kocha huyo amesema anaamini kibarua chake kilifika mwisho na hata akizungumza lolote kuhusiana na matokeo waliyokuwa wakiyapata haitakuwa na maana isipokuwa anaamini ukweli huwa haujafichi na kwa sasa anakubali lawama zote.
“Kikubwa nimeshaachana na timu na siwezi kuanza kuzungumzia yaliyopita ila kama kuna ukweli siku utajulikana lakini ipo wazi timu ikifanya vibaya lazima aangaliwe kocha, kwa hiyo niseme hilo nalibeba mimi kama kocha,” alisema Hitimana.
Kocha huyo aliyewahi kuinoa Simba pia amesema kwamba kwa sasa anatarajia kurejea kwao kupumzika kujipanga upya kwa ajili ya maisha mapya ya kwenye timu nyingine ingawa hajajua ni wapi ataelekea.
“Sijapata ofa kokote bado ni mapema lakini wiki ijayo nitarejea nyumbani Rwanda na kisha nitaangalia nini kinafuata. Timu yoyote nitazungumza nayo ikija lakini nitaangalia zaidi malengo yao kuliko ukubwa au umaarufu walionao,” alisema Hitimana.
