Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu NBC jana Jumanne umewapa nafasi ya kujiamini kuelekea mchezo wao na Simba utakaochezwa Jumapili hii.
Kaze alisema katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, wachezaji walionesha kiwango cha juu na kila mmoja alikuwa vizuri kuhakikisha wanapata matokeo bora.
“Uwezo wa wachezaji kutaka mafanikio katika mchezo huo ulikuwa wa juu, kila mtu alikuwa anakimbia, anafanya kazi yake na kuonesha mahusiano mazuri baina ya mmoja kwenda mwingine, hii kwetu ni faida kuelekea mechi ijayo,” alisema.
Alisema kushinda mechi kuelekea mchezo dhidi ya mtani wao ni vizuri kwa sababu watafanya maandalizi kwa kujiamini wakitambua umuhimu wa mchezo huo ambao iwapo watashinda itawahakikishia nafasi ya kutetea taji la Ligi Kuu NBC.
Ingawa alisema mechi dhidi ya mtani mara nyingi haitabiriki kwa sababu unaweza kuwa bora ukafungwa hata kama mwenzako anashika nafasi ya saba au ya mwisho.
“Derby haitabiriki hata kama uko bora, ni mechi tofauti na nyingine. Ni muhimu kwetu kurudi kujipanga kwa ajili ya mchezo tukijua hautakuwa rahisi,” alisema Kaze.
Kwa upande wake, kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime aliwapongeza wapinzani wake Yanga akisema walistahili kushinda kwas ababu walicheza vizuri kuliko wao.
“Mpinzani alikuwa juu, tulizidiwa, tulitegewa mtego tukanasa tutarudi kujiandaa kuangalia mechi zilizobaki na kujipanga kufanya vizuri zaidi,” alisema.
