Na Hassan Kingu
Michuano ya klabu Afrika ipo kwenye hatua ya robo fainali na timu za Tanzania zimefanikiwa kusonga kwenye hatua hiyo kati ya timu 16 zilizobaki kwenye michuano hiyo.
Simba imepangiwa kucheza na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Wydad Casablanca kutoka Morocco na kwenye Kombe la Shirikisho, Yanga itaumana na Rivers United ya Nigeria.
Ni michezo migumu kwa timu zote kutokana na uhalisia wa uyakinifu wa hatua hiyo kwa waliojitutumua kufika hapo huku zikiwa zimesalia mechi chache kabla ya kubainika bingwa mpya hivyo kila mmoja hutoa jicho, ufundi, utalaam, ujuzi na ubora wa hali ya juu ili kutimiza ndoto zake.
Simba na Yanga zimefanikiwa kufika hapo kwa kukusanya pointi za kutosha katika mechi sita za makundi zilizotokana na ushindi wa mechi zao kwa kufunga mabao ya kutosha.
Katika hatua ya makundi Simba imefunga mabao 10 na Yanga imefunga mabao tisa. Mabao yote ya Simba yamefungwa na wachezaji wa kigeni; Clatous Chama, Jean Baleke, Sadio Kanoute na Henock Inonga.
Mabao ya Yanga pia, saba yamefungwa na Fiston Mayele, Tuisila Kisinda, Kennedy Musonda na Jesus Moloko isipokuwa mawili pekee yaliyofungwa na wazawa Farid Mussa na Mudathir Yahya ambao wote waliwafunga TP Mazembe.
Hongera kwa Mudathir kuibuka mfungaji wa bao bora wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho akiwa ni mchezaji pekee wa Yanga kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Pamoja na kazi safi ya Mudathir lakini bado wachezaji wazawa wa Simba na Yanga wanapaswa kujiuliza shida ni nini? Timu za nyumbani kwao zinafanya vizuri lakini sio wao wanaofanya vema kwenye namba za magoli!
Katika orodha ya wafungaji bora wa Kombe la Shirikisho Msenegali, Paul Acquah wa Rivers ana mabao manne akiwa amefungana na Muivory Coast, Aubin Kouame wa Asec Mimosas ya nchini kwao na Ranga Chivaviro anayekipiga Marumo Gallants ya kwao Afrika Kusini.
Kisha wanafuatia, Mmisri Mostafa Fathi wa Pyramids (Misri), Mcongo, Malanga Mwaku (St. Lupopo, DRC), Boubacar Traore raia wa Mali anayekipiga US Monastir (Tunisia) na Mayele ambao wote wamefunga mara tatu.

Kwenye Ligi ya Mabingwa, Mmorocco Hamza Khabba wa Raja Casablanca (Morocco) anaongoza kwa mabao matano. Anafuatiwa na Mcongo, Makabi Lilepo wa Al Hilal (Sudan), Mmisri, Mahmoud Kahraba wa Al Ahly (Misri) na Chama waliofunga mabao manne kila mmoja.
Ukisoma kwa makini hiyo orodha, utagundua kwenye wengi waliopo hapo wanakipiga kwao na wanaiwakilisha nchi moja kwa moja lakini Tanzania utaona inawakilishwa na wageni.
Kwa kinachotokea kwa timu za Tanzania si dhambi lakini si jambo jema kwenye ukuaji wa soka la nchi na pia ni jambo la kuwafanya wachezaji wazawa kujiuliza kulikoni.
Ni kweli kwamba wachezaji wa kigeni wanapaswa kufanya kazi maradufu kwa sababu huduma na pesa wanazopata ni nyingi pia lakini hii haiwazuii wazawa kuonesha ubora wao, kulipigania taifa kupitia klabu ya nyumbani na mwisho ni mafanikio ya taifa unalotokea na mafanikio binafsi ya kwenda kukipiga kwingine na kutengeneza pesa zaidi.

Pia ni kama vile hili suala haliwasumbui wazawa, wanachukulia sawa tu wageni kuja kuchota pesa na kuondoka na rekodi za Afrika wakati wao wapo na wao ndiyo haswa uwakilishi wa Afrika unawahusu kwa timu za nyumbani.
Ukiachana na Afrika, hata ukienda Ulaya au Amerika kwenye ligi zao nyingi ‘homeboys’ wanachangamka kweli kweli kwenye orodha za mafanikio binafsi ya ligi bila ya kuangalia kiasi cha pesa wanacholipwa wala kupima mizani ya huduma anazopewa.
Kama upo kwenye timu inayoshiriki kimataifa, kwa nini usioneshe uwezo ukipewa nafasi? Usikubali kuwa mchezaji wa kuziba nafasi mwingine akiwa hayupo, ‘pambania kombe’.
Wazawa mnapaswa kuamka, bado mna nafasi na huu ndiyo wakati sahihi hasa kipindi hiki ambacho soka la Tanzania linapiga hatua kila dakika, msibaki nyuma, msikubali kupitwa na muda ambao ni wa kwenu na upo kwenye mikono yenu.
Hii inawahusu wanaocheza safu za ushambuliaji wa Simba, Kibu Denis, Habibu Kyombo, Mohamed Mussa na wengine ambao wanacheza nafasi nyingine lakini wana ustadi wa kufunga kama Jimmyson Mwanuke na Nassoro Kapama.
Pale Yanga kuna Dickson Ambundo, Denis Nkane, Crispine Ngushi, Clement Mzize ambaye angalau amekuwa akicheka na nyavu mara kwa mara kwenye michuano mingine lakini bado kuna nguvu inahitajika kuoneshwa hata kwenye michuano ya kimataifa inapotokea wamepata nafasi.
Muda mwingine maisha ya soka huwiana na maisha ya kawaida kwa maana ya unapopata nafasi itumie kikamilifu na kamia kutimiza lengo la msingi lililokuweka uwanjani maana huwezi kujua baada ya hapo matokeo yake yanakwenda kugusa wangapi.

Yawezekana mchezaji akaamini anafanya kwa ajili yake tu lakini pengine kupambana kwake sasa hivi kunaweza kuwa chachu ya kuwaaminisha vijana na watoto wengi ambao wanatamani kupata nafasi kama hizo lakini wana hofu juu ya wachezaji wa kigeni.
Hofu hii waanze kuondolewa kwa kuonesha mfano na kaka zao, wafute fikra potofu juu ya kushindwa kupambana na mgeni.
Kila kitu kinawezekana kama kutakuwa na nia kweli na hasira ya mafanikio. Miaka ya nyuma, iliaminika kutoka kimpira lazima uzunguke kwenye mataifa mengine Afrika, ni kweli lakini sasa angalau unaweza kutoboa ukiwa hapa hapa Tanzania.
Mifano mingi tunayo, haina haja ya kuanza kuwataja kina Novatus Dismas na wengine lakini ifahamike wakati ndiyo huu, biashara ya soka Tanzania kwa sasa imeanza kuwa kubwa, sasa kwa nini wazawa tusinyanyuke nayo?
