Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kally Ongala amesema siri ya ushindi wao dhidi ya Mtibwa Sugar ni wachezaji wake kuutawala mchezo na kufuata vyema maelekezo aliyowapa .
Azam jana iliungana na Singida Big Stars kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA (ASFC), baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Kocha huyo alikiri kuwa timu yake haikucheza vizuri hasa kipindi cha kwanza lakini nidhamu iliyooneshwa na wachezaji wake na ushindi walioupata imemfanya ajisikie furaha.
“Tulicheza pungufu kwa dakika 70 lakini nawapongeza wachezaji wangu kwa kuwaheshimu Mtibwa na kucheza kwa nidhamu muda wote wa dakika 90, naamini pamoja na kuwa pungufu lakini tulistahili kushinda,” alisema Kally.
Kocha huyo ameeleza kuwa baada ya ushindi huo wanarudi kwenye uwanja wa mazoezi kuangalia mapungufu yao ili kuyarekebisha na kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao lengo likiwa ni kufanya vizuri na kusonga hatua inayofuata.
Alisema anatambua kuwa hatua inayofuata itakuwa ngumu zaidi lakini dhamira yao msimu huu ni kuwa mabingwa wa Kombe la FA hivyo watajipanga vizuri na kurekebisha mapungufu yao ili kushinda mchezo huo.
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga ameeleza kuwa kipigo walichokipata kutoka kwa wapinzani wao kimetokana na makosa ambayo waliyafanya ikiwemo kushindwa kutumia faida ya wapinzani wao kuwa pungufu uwanjani.
“Tumepoteza mchezo kwa uzembe wetu wenyewe, tulifanya makosa wenzetu wameyatumia, lakini hata sisi tulitengeneza nafasi tukashindwa kuzitumia kitu ambacho kimetugharimu na kujikuta tunatolewa kwenye mashindano,” alisema Mayanga.
Kocha huyo ameeleza kuwa wamekubali matokeo na wanarudi kujipanga kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya mwaka ujao .
