Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema amefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na timu yake licha ya kufungwa mabao 3-1 na Raja Casablanca.
Simba ilipoteza mchezo huo wa mwisho wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Mohamed V, Casablanca usiku wa kuamkia leo lakini ikiwa tayari imefuzu hatua ya robo fainali.
Baada ya kipigo hicho Simba hata hivyo imemaliza katika nafasi ya pili katika kundi yale ikiwa na pointi tisa, Raja ikiwa kileleni baada ya kujikusanyia pointi 16.
Robertinho alisema amefurahishwa na wachezaji wake namna walivyocheza kwa kufuata mbinu mpya walizojifunza ambazo walikuwa wanazijaribu kwenye mchezo huo kwa ajili ya robo fainali.
“Mipango imefanya kazi vizuri kwenye mechi, tuliudhibiti mchezo na tukafunga bao, timu yetu ilikuwa inatoa kipaumbele kwa mchezaji mwenye mpira na hata ushambuliaji wa Baleke (Jean) ulikuwa tofauti na ilivyozoeleka.
“Tumefanya hivyo kwa sababu tuna michezo mipya migumu mbele yetu, na wachezaji wameonesha tuna wakati ujao mzuri, niko Simba kwa miezi minne sasa, nimeliona hilo na nitaweka alama zangu kwenye eneo hilo,” alisema Robertinho raia wa Brazil.
Naye ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally ameieleza GreenSports kuwa timu hiyo imeondoka leo Morocco saa 10 jioni ikipitia Uturuki kabla ya kuelekea Ethiopia, wakitarajia kutua Dar es Salaam saa tano asubuhi ya kesho.
“Kila kitu kipo sawa, tumemaliza mechi salama na tunaangalia namna ya kuondoka, tutaondoka saa 10 jioni ya leo kisha tutakwenda Uturuki na huko tutaunganisha mpaka Ethiopia na tunatarajia kuwepo Dar es Salaam majira ya saa tano asubuhi,” alisema Ally.
Simba sasa inasubiri kuchezeshwa kwa droo ya robo fainali ya michuano hiyo ambapo mechi za hatua hiyo zinatarajia kupigwa Aprili 21 na mechi za marudiano Aprili 28, mwaka huu.
