Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema licha ya timu ya taifa, Taifa Stars kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Uganda lakini wachezaji wanapaswa kupongezwa kwa kazi waliyoifanya.
Maxime ameeleza hayo akisisitiza kuwa mbali na matokeo hayo lakini vijana walijitahidi kupambana na kwamba haikuwa riziki yao na ushindi ukatua kwa Uganda.
Alisema kuwa wanapaswa kupongezwa na si kukatishwa tamaa kwani bado kuna nafasi ya mechi mbili za kufanya vizuri kufuzu kushiriki fainali za Mataifa Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyika Ivory Coast.
“Inabidi tuwapongeze, wamepambana kwa kiasi chao lakini yote kwa yote haikuwa riziki yetu, wao (Uganda) wamepata matokeo lakini kikubwa ni kuwapongeza wachezaji maana bado wana nafasi, tuna mechi mbili tusikate tamaa,” alisema Maxime nahodha wa zamani wa Stars.
Alisema kiufundi timu hiyo ilipoteza mchezo huo uliopigwa juzi Jumanne, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam baada ya kutoka kwa viungo Mzamiru Yassin na Himid Mao ambao kwa kiasi kikubwa walifanikiwa kuidhibiti Uganda eneo la katikati ambalo walikuwa hatari zaidi.
Katika Kundi F, Stars inashikilia nafasi ya pili kwa pointi nne sawa na Uganda inayoshika nafasi ya tatu. Algeria imeshafuzu kwa pointi zake 12 ikiwa kileleni huku Niger ikiburuza mkia kwa pointi mbili.