Na mwandishi wetu
Kikosi cha Simba kimeendelea leo na safari yake ya kuelekea Morocco kwa mechi yao na Raja Casablanca baada ya jana kukwama kusafiri kutokana na hitilafu ya ndege waliyopanda.
Simba ilianza juzi safari yake hiyo kwenye Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kupitia Kilimanjaro ambapo walipofika hapo ndege hiyo ilipata hitilafu na kulazimika kulala mpaka jana.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alieleza kuwa safari hiyo ya kupitia Qatar kuelekea Morocco imeanza jana saa tano asubuhi.
“Kulikuwa na hitilafu ya ndege tulipofika Kilimanjaro, hivyo tumelala hapa na saa tano tunatarajia kuanza safari ya kuelekea Morocco kupitia Qatar tayari kwa ajili ya mechi na Raja, na kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa,” alisema Ally.
Simba wameondoka na kikosi cha wachezaji 13 huku wachezaji wengine ambao wanaotumikia timu zao za taifa wakitarajia kujiunga moja kwa moja Morocco.
Mchezo huo na Raja wa kukamilisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika unatarajia kupigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mohamed V, Casablanca.
Simba tayari imeshafuzu hatua ya robo fainali baada ya kufikisha pointi tisa zilizowaweka kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa Kundi C ambalo linaongozwa na Raja yenye pointi 12.
