London, England
Kocha wa England, Gareth Southgate amesema mshambuliaji wa timu hiyo, Bukayo Saka ameendelea kuwa mwenye ‘shauku ya ajabu’ ya mafanikio jambo linalosaidia kupandisha kiwango chake msimu huu.
Saka ambaye pia anaichezea Arsenal, jana Jumapili aliisaidia England kupata bao la kwanza kabla ya yeye mwenyewe kufunga la pili wakati timu hiyo ikiilaza Ukraine mabao 2-0.
Huo unakuwa ushindi wa pili mfululizo kwa England kwenye michuano ya kuwania kufuzu fainali za Euro 2024 ikiwa tayari imeanza na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Italia Alhamisi iliyopita.
Katika mechi ya jana, England ilipata bao lake la kwanza kupitia kwa nahodha wa timu hiyo, Harry Kane akiitumia vizuri krosi ya Saka, hilo likiwa ni bao la 55 kwa Kane akiwa na England.
Saka alikamilisha bao la pili baada ya kuinasa pasi ya Jordan Henderson na kuonyesha uwezo binafsi kabla ya kuujaza mpira wavuni, hilo likiwa bao lake la 17 msimu huu akiwa na Arsenal na England.
“Hiyo ni ‘shauku ya ajabu’ ambayo imeongezeka katika soka lake kwa kipindi cha miezi 18 au zaidi iliyopita, kuna wakati usingekuwa na uhakika kama atafunga lakini kwa sasa ana ile hali ya kujiamini mbele ya goli,” alisema Southgate akimzungumzia Saka ambaye ndio kwanza ana miaka 21.
“Nafikiri kwa sasa anapokuwa mbele ya goli anacheza akiwa na uhakika, hilo lipo wazi katika klabu, na limeonekana katika mechi zetu, kwa sasa unamtegemea lazima afunge, na hiyo ni mabadiliko ya kifikra kuliko mbinu kwani tayari ni mchezaji mwenye mbinu,” aliongeza Southgate.
Baada ya kuiwakilisha England, Saka atarejea dimbani Jumamosi hii na jezi ya Arsenal katika Ligi Kuu England dhidi ya Leeds wakati Arsenal ikipigania pointi tatu muhimu za kujiimaisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Matokeo ya mechi za kufuzu Euro 2024 za jana Jumapili ni kama ifuatavyo…
Kazakhstan 3-2 Denmark
England 2-0 Ukraine
Luxembourg 0-6 Portugal
Malta 0-2 Italia
Northern Ireland 0-1 Finland
Liechtenstein 0-7 Iceland
Slovenia 2-0 San Marino
Slovakia 2-0 Bos-Herze
Mechi za kufuzu Euro 2024 zitakazochezwa leo Jumatatu ni kama ifuatavyo…
R. of Ireland v Ufaransa
Uholanzi v Gibraltar
Moldova v Jamhuri ya Czech
Poland v Albania
Austria v Estonia
Sweden v Azerbaijan
Hungary v Bulgaria
Montenegro v Serbia
