Buenos Aires, Argentina
Lionel Messi amepewa heshima nchini Argentina baada ya chama cha soka nchini humo kutangaza uwanja wa mazoezi wa timu ya Taifa kuitwa kwa jina la mchezaji huyo.
Messi ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa ya Argentina ambayo Desemba mwaka jana aliiongoza kubeba Kombe la Dunia, tangu mwaka 2005 hadi sasa ameichezea timu hiyo mara 173.
Rais wa Chama cha Soka Argentina, Claudio Tapia, kocha wa timu ya Taifa ya nchi hiyo, Lionel Scalloni na Messi mwenyewe, juzi Jumamosi walishiriki hafla ya uzinduzi wa jina hilo yalipo makao makuu ya timu ya taifa.
“Leo tunashuhudia tukio la kihistoria katika eneo hili, ambalo kuanzia sasa hapa patajulikana kwa jina la Lionel Andres Messi, kwa heshima ya mchezaji bora duniani,” alisema Tapia.
Makao makuu ya timu hiyo ambapo pia ndipo kwenye uwanja wa mazoezi wa timu hiyo, ni eneo lililo umbali wa kilomita 40 kutoka katikati ya jiji maarufu la Buenos Aires nchini Argentina.
Messi ambaye Alhamisi iliyopita wakati akiiwakilisha Argentina katika mechi ya kirafiki na Panama, alifunga bao lake la 800 katika maisha yake ya soka la ushindani, aliguswa mno na tukio la uzinduzi huo.
“Nimekuwa nikija hapa kwa miaka 20 na wakati wote nimekuwa nikijiona mwenye nguvu mpya, hili ni jambo la kufurahisha kwangu, nina furaha sana, hii ni heshima ya kipekee,” alisema Messi.
“Hili ni eneo la aina yake, hata katika kipindi kigumu ambacho nami huwa napitia, nimekuwa nikija hapa na kusahau kila kitu, naweza kuja hapa na kujisikia furaha kwa kuwa kwenye eneo hili na bado naona hivyo, na ndio maana najisikia raha kweli kwamba baada ya siku nyingi hatimaye mahali hapa panapewa jina langu,” alisema Messi.
Messi, nyota wa zamani wa Barcelona ambaye kwa sasa anaichezea PSG ya Ufaransa, ni mshindi wa tuzo za Ballon d’Or kwa mara saba.
