Na mwandishi wetu
Klabu ya Azam FC imesema inatafuta kasi kujiweka imara kwa ajili ya mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (Kombe la FA) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa mwezi ujao.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Ofisa Habari wa Azam, Hasheem Ibwe alisema katika kujiweka imara watacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC keshokutwa wakiamini ni kipimo sahihi kuelekea kwenye mchezo huo utakaochezwa Azam Complex, Dar es Salaam.
“Tumeona kabla ya kucheza mchezo wetu wa robo fainali, tutafute uimara wa timu, Jumatatu tutacheza mchezo wa kujipima nguvu na KMC ili kujiweka vizuri kwa mchezo ujao wa FA,” alisema Ibwe.
Alisema hali za wachezaji ziko vizuri na kila mtu anajua umuhimu wa mchezo huo wa FA kwamba wanahitaji kusonga mbele hivyo watajipanga kulingana na aina ya mpinzani waliyenaye.
Tayari Azam imeshacheza mchezo mmoja wa kirafiki na JKU ya Zanzibar na kushinda mabao 2-0. Mshindi kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar anatarajiwa kucheza hatua ya nusu fainali na mshindi kati ya Simba na Ihefu.
