Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba leo Alhamisi imesaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 500 milioni na Kampuni ya MobiAd Afrika kwa ajili ya kukuza na kuendeleza soka la timu za vijana wa klabu hiyo.
Mkataba huo umesainiwa hii leo na kushuhudiwa na viongozi wa pande zote mbili katika hafla ndogo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula amesema: “Soka la vijana ni muhimu sana. Ili uwe na timu ya vijana iliyo bora lazima iwezeshwe. Kama ilivyo kwa wachezaji wengine.
“Simba inakwenda mbele kutambua vipaji, kuvichukua na kuviendeleza na kutengeneza timu yenye vipaji vikubwa sana. Tunaamini Simba imara yenye vipaji haitaisaidia Simba pekee bali hata taifa letu,” alisema.
“Yawezekana wachezaji tunaowaona ni sababu ya bahati, lakini tunatengeneza mfumo ambao kila kijana mwenye kipaji tutamwezesha kukuza kipaji chake, lakini si tu kuendeleza kipaji cha mpira lakini pia kusoma shule.”
Naye Mtendaji Mkuu wa MobiAd, Lumisho Sikoni, alisema anaishukuru Simba kwa kuwapa nafasi ya kufanya nao kazi kwani vijana ni taifa la kesho hivyo matayarisho yao yanapaswa kuanza leo na wakaona ni wakati sahihi wa kuanza safari pamoja na Simba.
“Ni safari ndefu ambayo inahitaji mshikamano, tuna mategemeo chanya na huu ni mwanzo tu kuna udhamini mkubwa unakuja tumeamua kufanya kazi na Simba ni timu kubwa barani Afrika ambayo iko mstari wa mbele katika kukuza soka la vijana,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema: “Hakuna miujiza kwenye soka, ili kupata timu nzuri unapaswa kuwekeza kwa vijana.”
“Tunaamini pesa hizi zitatimiza malengo yenu na yetu, maana Simba ina malengo ya kuchochea soka la vijana, inaenda kutengeneza shamba la kuvuna wachezaji vijana,” alisema Try Again.
