Na mwandishi wetu
Simba leo Jumamosi imetinga kibabe hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuinyuka Horoya ya Guinea mabao 7-0 katika mechi ya hatua ya makundi.
Ushindi huo mnono pia umeifanya Simba kulamba kitita cha Sh 35 milioni kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyeahidi ‘kununua’ kila bao kwa sh 5 milioni, hiyo ni mbali na mamilioni ya CAF.
Kwa mara nyingine, Clatous Chota Chama au Mwamba wa Lusaka alidhihirisha umahiri wake si kwa kupika mabao bali kwa kufunga, ametupia kambani mabao matatu (hat trick) na kuondoka na mpira.
Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Jean Baleke aliyefunga mawili, Pape Sakho na Sadio Kanoute ambao kila mmoja alifunga bao moja.
Katika mechi hiyo, Chama (pichani juu) anabaki kuwa mpishi na mfungaji muhimu aliyefanya kazi nzuri, hakuwa mbinafsi wa kutoa pasi lakini alipoona anaweza kufunga hakusita kufanya hivyo.
Mabao yote ya Chama yalikuwa burudani alionyesha uwezo wake, kujiamini, hakuwa mwenye papara karibu na lango na mabao yake yote yalikuwa burudani kwa mashabiki wa Simba.
Ushindi huo sasa unaifanya Simba iliyo Kundi C kushika nafasi ya pili ikiwa imefikisha pointi tisa ikitanguliwa na Raja Casablanca inayoshika usukani ikiwa na pointi 13.
Vipers, timu iliyoonekana kibonde katika kundi hilo inashika nafasi ya nne ikiwa na ponti mbili lakini leo imegawana pointi na wababe wa kundi hilo Raja ambao hata hivyo walicheza mechi hiyo wakiwa tayari wamefuzu robo fainali.
Horoya iliyokumbana na kipigo cha mbwa koko mbele ya Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa imekusanya pointi nne.
Kimataifa Simba yatinga robo fainali kibabe
Simba yatinga robo fainali kibabe
Read also
