Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke amejinasibu kuwa yeye ndiye mshindani halisi wa Fiston Mayele wa Yanga, katika mbio za kuwania ufungaji bora kwenye Ligi Kuu NBC msimu huu.
Baleke ambaye ameifungia timu yake mabao matano katika mechi nne za Ligi Kuu alizoichezea Simba, alisema kufunga ndio kipaji chake na huwa hajisikii vizuri anapotoka uwanjani hajafunga bao.
“Kama ningeanza na timu mwanzo wa msimu ningekuwa nimempita kwa idadi ya mabao Mayele, sababu kwenye timu yangu kuna viungo wengi wanaojua kutengeneza nafasi lakini kingine mimi mwenyewe napenda kufunga, huwa najisikia vibaya kama sijatimiza jukumu langu nikitoka uwanjani bila bao,” alisema Baleke.
Mshambuliaji huyo ameeleza kuwa kwa msimu ujao atafanya mambo makubwa na kudhihirisha hicho anachokisema kwa kuifungia timu yake ya Simba mabao ya kutosha na yeye kubeba tuzo hiyo ambayo kwa msimu huu huenda ikachukuliwa na Mayele.
Alisema anaujua uwezo wa Mayele tangu wakiwa kwao DR Congo akidai ni mshambuliaji mzuri kwenye kufunga lakini angehakikisha anapambana naye ili kuisaidia timu yake na kuonesha uwezo aliokuwa nao katika kufunga.
Baleke amejiunga na Simba kwenye dirisha dogo msimu huu akitokea TP Mazembe ya DR Congo na tayari ameifungia timu hiyo ‘hat-trick’ (mabao matatu) moja katika mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar katika ushindi wa mabao 3-0.
