Madrid, Hispania
Rais wa La Liga, Javier Tebas amesema anajisikia aibu kwa mgogoro unaoshusha heshima ya soka Hispania wakati huu Barcelona ikituhumiwa kutoa malipo yanayotiliwa shaka kwa makamu rais wa kamati ya waamuzi.
Waendesha mashitaka Hispania wiki iliyopita walidai kwamba Barca ilitaka upendeleo kwa waamuzi kwa makubaliano ambayo klabu hiyo ilimlipa makamu rais wa kamati ya waamuzi, Jose Maria Negreira Euro milioni 7 kati ya mwaka 2001 na 2018.
Kashfa hiyo imeibua sintofahamu nchini Hispania huku baadhi ya mashabiki wakilalamikia tukio hilo katika mechi za soka za mwishoni mwa wiki kwa kurusha noti feki uwanjani.
Barca hata hivyo imedai kwamba ilimlipa Negreira kwa ajili ya ripoti ya ufundi kuhusu waamuzi ingawa Tebas hakubaliani na hoja hiyo akidai klabu hiyo na rais wao, Joan Laporta hawalishughulikii jambo hilo vizuri.
“Najisikia aibu kwa kuwa bado hatujapata maelezo yanayojitosheleza, ukweli ni kwamba bado hatujapata maelezo yoyote kutoka Barcelona na hili litachukua muda kuliweka sawa,” alisema Tebas jana Jumatatu.
“Sikumbuki kutokea mgogoro unaoshusha heshima kama huu, tunatakiwa kuliangalia jambo hilo hadi mwisho wake, kuna malipo yamefanyika na hilo ni jambo ambalo Barcelona wamekiri, hiki si kitu cha kawaida,” alisema.
“Inaeleweka kwamba kuna hali ya sintofahamu imeibuka kutokana na jambo hili, na hapa si tu kwamba tunahofu ya kushusha hadhi na heshima ya Barca bali ni hivyo hivyo kwa hadhi na heshima ya mashindano,” aliongeza.
Wakati huo huo, Baraza la Juu la Michezo Hispania (CSD) nalo limeibuka kuthibitisha kwamba litakuwa tayari kuungana na waendesha mashitaka kuhusu tuhuma za Barca kumlipa fedha Negreira.
Juzi Jumapili, klabu ya Real Madrid ilitangaza kwamba itakuwa tayari kutoa ushirikiano katika kesi hiyo ili kulinda hadhi na heshima yake.
Akizungumzia tuhuma hizo, Rais wa Barca, Joan Laporta (pichani juu) alisisitiza kuwa klabu yake haijafanya kosa lolote na kuahidi kukabiliana na wale wote wanaojaribu kuharibu hadhi ya klabu hiyo.
“Barca ni klabu yenye miiko yake, hatutumii maneno ili kuonekana tuko safi badala yake ni miiko yetu tunayoshikamana nayo ambayo ni sehemu ya umahiri wetu katika michezo, na ndio maana Barca inaonewa wivu na inafahamika kote duniani,” alisema.
“Hiyo pia inamaanisha kwamba kuna wanaoshawishiwa kwa wivu wao kujaribu kushusha hadhi yetu kwa kuendesha kampeni zenye nia mbaya, wana rundo la mashambulizi yenye lengo la kuharibu taswira ya klabu, mashambulizi ambayo hayana ukweli wowote,” aliongeza Laporta.
“Uhakika ni kwamba bodi itaitetea klabu kwa nguvu zetu zote, na kimsingi ninataka kukabiliana na hao watu wasio na aibu, ambao wanajaribu kuiharibu hadhi ya klabu,” alisema Laporta.
