Na mwandishi wetu
Simba imeendelea kuimarisha mbio za kuishusha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya kutamba ugenini kwa kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa Jumamosi hii.
Kwa matokeo hayo, Simba sasa imefikisha pointi 57 katika mechi 24 ikizidiwa na mahasimu wake Yanga kwa pointi tano lakini imeboresha mabao ya kufunga yakifikia 58 dhidi ya 42 ya Yanga.
Kwa hesabu zilivyo Simba sasa inaombea Yanga ipoteze japo mchezo mmoja au itoke sare mbili ili timu hizo mbili zitakapokutana iitumie mechi hiyo kuweka mambo sawa ikitarajia kunufaika na mtaji wa mabao mengi ya kufunga.
Yanga Jumapili hii itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Geita Gold, mechi ambayo inalazimika kushinda ili kuzidi kuikatisha tamaa Simba, vinginevyo ikipata matokeo mabaya itakuwa imezidi kufufua matumaini ya Simba kuishusha kileleni.
Aliyeimarisha mbio za Simba kuishusha Yanga kileleni alikuwa ni mshambuliaji Jean Baleke kutoka DR Congo ambaye ndiye aliyefunga mabao yote matatu (hat trick) ya Simba.
Baleke (pichani juu) alifunga bao la kwanza dakika ya tatu tu ya mchezo huo akiitumia pasi ya Moses Phiri lakini kabla Mtibwa hawajajipanga kujua watasawazisha vipi walijikuta wakifungwa bao la pili dakika nne baadaye.
Safari hii Baleke, alifunga bao hilo kwa kichwa akiitumia vizuri krosi iliyochongwa na Saido Ntibazonkiza ikitokana na pasi fupi ya kona iliyoanzia kwa Clatous Chama.
Baleke alikamilisha karamu ya mabao kwa Simba dakika 10 kabla ya timu hizo kwenda mapumziko akimalizia pasi ya beki Shomary Kapombe.
Kwa mabao hayo, Baleke sasa anakuwa amefikisha jumla ya mabao matano lakini hapo hapo ameweka rekodi ya kufunga hat trick yake ya kwanza katika Ligi Kuu NBC tangu asajiliwe na Simba katika dirisha dogo la usajili miezi takriban miwili iliyopita.
Katika mechi hiyo, wenyeji Mtibwa hawakuonyesha makali yoyote ya kuitisha Simba ambayo ushindi huo unazidi kuwaimarisha katika kuhakikisha wanawaweka pabaya mahasimu wao Yanga.
Simba kama ilivyo Yanga wote wana vibarua vigumu kwenye michuano ya Afrika, Simba ikishiriki Ligi ya Mabingwa na Yanga Kombe la Shirikisho, hapo hapo Yanga inataka kulitetea taji la Ligi Kuu NBC kama Simba inavyotaka kuipora Yanga taji hilo.
Soka Simba yaikomalia Yanga kileleni
Simba yaikomalia Yanga kileleni
Read also
