Na Hassan Kingu
Leo, Jumanne saa moja usiku, Simba wanaumana na Vipers ya Uganda katika mechi ambayo ni lazima washinde ili washike nafasi ya pili au wajiweke mguu sawa kuelekea robo fainali. Tofauti na hivyo hali itakuwa tete.
Baada ya ushindi wa kwanza wa bao 1-0 ugenini Uganda, leo Simba ikiwa nyumbani kwenye dimba la Benjamin Mkapa ushindi utaihakikishia pointi tatu zinazoweza kuwapaisha hadi nafasi ya pili pamoja na kuwaweka pazuri katika kuwania tiketi ya robo fainali.
Ushindi wa leo bila kujali matokeo ya Raja Casablanca na Horoya ambazo zitaumana saa nne usiku, utakuwa na maana kubwa kwa Simba, watafikisha pointi sita na kuwa mbele ya Horoya yenye pointi nne.
Horoya inaweza kuipiku Simba na kujiimarisha katika nafasi ya pili iwapo itaifunga Raja na kufikisha pointi saba, matokeo ambayo yataifanya Simba ibaki nafasi ya tatu lakini ikiwa na faida ya ushindi wa mechi yake na Vipers.
Ushindi wa Horoya kwa Raja pia hauwezi kuiondoa Simba katika matumaini ya kukata tiketi ya robo fainali kwani bado inasubiri kuumana na timu hiyo tena nyumbani na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kulipa kisasi baada ya kushindwa kutamba ugenini, Guinea.
Kwa upande mwingine iwapo Simba leo itapoteza mechi na Vipers itajiweka pagumu na kufifisha matumaini yaliyoanza kuibuka, itashika mkia, Vipers itafikisha pointi nne na kushika nafasi ya tatu.
Mazingira ya aina hiyo ndiyo yanayoifanya Simba ihakikishe kwa namna yoyote ile inapata ushindi hii leo, ile hadithi ya Kwa Mkapa hatoki mtu na iwe hivyo leo katika mechi dhidi ya Vipers.
Kwa msimamo na mwenendo wa Kundi C, dalili zote zinaonyesha kuwa Raja ni timu ngumu, hivyo ni lazima Simba ihakikishe inacheza vyema karata zake katika mechi dhidi ya Vipers na baadaye Horoya.
Faida iliyonayo Simba ni kwamba tayari imedhihirisha hilo, imeshaifunga Vipers ugenini na ingawa imepoteza kwa Horoya bado ina nafasi ya kujibu mapigo nyumbani kwenye dimba la Kwa Mkapa.
Raja ndiyo inayoshika usukani wa kundi hilo ikiwa na pointi tisa, haijapoteza mchezo hata mmoja, ikifuatiwa na Horoya yenye pointi nne na Simba yenye pointi tatu. Vipers inashika mkia na pointi yake moja.
Kimataifa Simba ushindi lazima, vinginevyo…
Simba ushindi lazima, vinginevyo…
Read also
