Na mwandishi wetu
Beki wa Mtibwa Sugar, Iddy Mobby Mfaume amefariki dunia leo Jumapili mchana katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma alikokuwa akipatiwa matibabu.
Ofisa habari wa Mtibwa, Thobias Kifaru amesema Mobby amefariki baada ya kupata tatizo la kiafya jana Machi 4, Morogoro wakati akiwa kwenye mazoezi binafsi pembezoni mwa barabara kuelekea mchezo wao wa Kombe la FA dhidi ya KMC uliopigwa leo.
Katika mechi hiyo iliyomalizika jana jioni Mtibwa ilishinda kwa bao 1-0 na kutinga hatua ya robo fainali ya michuanp hiyo.
“Baada ya kupata tatizo hilo kidogo tukampeleka hospitali ya kiwanda cha Sukari Mtibwa, Manungu lakini wakatuelekeza tumpeleke Hospitali ya Mission, tukafanya hivyo lakini nao pia wakatuambia anahitaji vipimo vikubwa zaidi.
“Ndipo sasa ikabidi tumpeleke Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma na tukafika saa 7 usiku, na kuanza kuchukuliwa vipimo mbalimbali vikaendelea na leo ikawa ametutoka na sasa tunafanya taratibu za mazishi ambayo yanatarajia kufanyika Shinyanga,” alisema Kifaru.
Mobby alitua Mtibwa Sugar msimu huu akitokea Ruvu Shooting lakini pia aliwahi kuzitumikia timu za Geita Gold, Polisi Tanzania, Stand United na Mwadui FC kwa nyakati tofauti na pia aliwahi kuitwa mara kadhaa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Soka Beki Mtibwa Sugar afariki dunia
Beki Mtibwa Sugar afariki dunia
Read also
