Barcelona, Hispania
Kocha wa Barcelona, Xavi Hernandez amesema lawama anazozipata baada ya timu yake kuifunga Real Madrid bao 1-0 inadhihirisha ni kwa nini yeye ni kocha wa klabu ‘ngumu kuiongoza duniani’.
Bao la kujifunga la Eder Militao liliiwezesha Barca kutoka na ushindi huo mwembamba dhidi ya Real Madrid timu hizo zilipoumana Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Katika mechi hiyo ya nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Mfalme, Xavi analaumiwa kwa kuwa Barca ilimiliki mpira kwa asilimia 35 tu, kiwango ambacho ni cha chini mno kwa takriban misimu minane iliyopita.
“Kidogo inaleta mkanganyiko, na ndio maana nasema Barcelona ni klabu ngumu duniani kuiongoza,” alisema Xavi wakati timu yake ikijiandaa kwa mechi ya La Liga dhidi ya Valencia leo Jumapili jioni.
“Ushindi pekee hapa hautoshi, unaifunga Real Madrid 1-0 na haiwavutii watu kwa sababu hujamiliki mpira kwa sana, lakini kwa upande mwingine ni sherehe ya kitaifa,” alisema Xavi.
“Nilisema hili msimu uliopita na nikashambuliwa, hapa Barca unatakiwa ushinde na uwe kivutio. Hili ndilo lengo letu lakini tulikuwa tunacheza na bingwa wa La Liga, vinara wa Ligi ya Mabingwa, kama wanakupeleka mbio kunakuwa na ugumu,” alisema Xavi.
“Kuzungumzia umiliki wa mpira wakati wenzako wanacheza mtu na mtu ni jambo la ajabu, hatukupanga kukaa na kujihami kwa chini, Real Madrid ndio waliotufikisha hapo, na ndivyo soka lilivyo,” alisema Xavi.
“Hii ni klabu ngumu zaidi duniani, hilo halina shaka, kuna mtazamo ulio wazi wa namna ya kucheza na kama hutofanya hivyo watu hawaridhiki, tumeshinda katika uwanja mgumu mno,” aliongeza Xavi.
Barca licha ya kutolewa katika Europa Ligi, wapo vizuri kwenye mbio za kushinda mataji matatu msimu huu, tayari mkononi wana taji la Super Cup (Hispania), wanaongoza La Liga kwa tofauti ya pointi saba na hivyo wana nafasi ya kulibeba taji hilo.
Kwenye Kombe la Mfalme bado wana nafasi ya kufanya vizuri katika mechi ya marudiano ambayo itachezwa Aprili 5 na Barca watakuwa kwenye dimba lao la nyumbani, Nou Camp.
