Na mwandishi wetu
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemtangaza aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Kenya, Adel Amrouche kuwa kocha mkuu mpya wa Taifa Stars.
TFF imelieleza hilo mchana huu kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram huku ikifafanua kuwa kwa muda wote ambao Amrouche atainoa Stars atakuwa akilipwa mshahara na Serikali.
Amrouche, 58 raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria mwenye uzoefu mkubwa wa soka la Afrika ametua kurithi mikoba ya Kim Poulsen aliyeondolewa baada ya timu kufanya vibaya katika michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).
Kocha huyo aliyewahi kuinoa timu ya taifa Kenya ‘Harambee Stars’ alitwaa tuzo ya Kocha Bora wa Afrika Mashariki mwaka 2013 baada ya kuipa timu hiyo ubingwa wa Cecafa Challenge na kabla ya hapo akiwa na Burundi alifika nusu fainali ya michuano hiyo mara mbili.
Akiwa na Harambee pia aliwahi kuweka rekodi ya kucheza mechi 20 bila kupoteza. Pia amewahi kuwa kocha wa timu za taifa za Guinea ya Ikweta, Botswana, Libya na Yemen kwa nyakati tofauti.
Amrouche hata hivyo alitimuliwa na Shirikisho la Soka Kenya na kushitaki Fifa akidai shirikisho hilo lilimtimua kimakosa na Fifa kuamua alipwe Sh 110 milioni za Kenya sawa na takriban Sh bilioni mbili za Tanzania.
Kocha huyo pia amewahi kufundisha ngazi za klabu ambapo aliinoa DC Motema Pembe ya DR Congo aliiwezesha kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika akiwa ameipa mara mbili ubingwa wa DR Congo na DRC Super Cup.
Timu nyingine alizowahi kuzinoa ni RC Kouba, USM Alger na MC Algiers zote za Algeria huku pia akiwa ni mkufunzi wa walimu wa Pro Licence wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) akizalisha makocha wengi bora barani Afrika.
Amrouche pia ni kocha mwenye uzoefu mkubwa katika soka la vijana, kazi aliyoifanya kwa zaidi ya miaka 10 nchini Algeria na Ubelgiji.
Ilifafanuliwa zaidi kuwa Amrouche anazungumza lugha za Kiarabu, Kifaransa, Kingereza na Kiswahili na kwa nyakati tofauti amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na Michezo katika klabu za Ubelgiji na Ukraine.
Amrouche ni kocha mwenye Uefa Pro Licence na Shahada ya Uzamili katika kuwasoma watu na Utimamu (Masters in Ergonomics in Physical Activity), amekuwa akifanya kazi za ukufunzi pia kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) katika kuzalisha walimu wa soka.
Kimataifa Amrouche kocha mpya Stars
Amrouche kocha mpya Stars
Read also
