Manchester, England
Wakala wa mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland aitwaye Rafaela Pimenta ameinadi Real Madrid akisema kwamba klabu hiyo ni ndoto ya kila mchezaji kujiunga nayo.
Kauli ya wakala huyo inatoa ishara kwamba haitokuwa ajabu siku moja Haaland akijiunga na timu hiyo hasa kutokana na mafanikio ambayo anaendelea kuyapata akiwa Man City.
Haaland mwenye umri wa miaka 22 tangu ajiunge na Man City majira ya kiangazi mwaka jana akitokea Borussia Dortmund, hadi sasa amefunga mabao 33 katika mechi 33, kati ya mabao hayo 27 ameyafunga kwenye Ligi Kuu England (EPL).
Habari za Haaland kujiunga na Real Madrid hapo baadaye si ngeni, iliwahi kudaiwa kuwa katika mkataba wake kuna kipengele kinachompa nafasi ya kujiunga na timu hiyo mwaka 2024 jambo ambalo kocha wake Pep Guardiola aliwahi kulikanusha siku za nyuma.
“Kuna Ligi Kuu England na hapo hapo kuna Madrid, timu yenye kitu fulani chakwake na pia ni timu ndoto ya kila mchezaji,” alisema Pimenta.
“Madrid wana maajabu wanayoyaendeleza, hawana mashindano ya kila wiki lakini wana Ligi ya Mabingwa Ulaya,” aliongeza Pimenta.
Pimenta ambaye ni mwanasheria kutoka Brazil pia ni mshirika wa kibiashara wa wakala Mino Raiola na amebeba jukumu la kuiendeleza kazi hiyo tangu kufa kwa Raiola Aprili mwaka jana.
Kwa mujibu wa Pimenta, Haaland alitaka kujiunga na Man City kwa sababu ya kutaka fursa ya kufanya kazi na Guardiola, mvuto wa EPL pamoja na ukweli kwamba baba yake mzazi Alfie naye aliwahi kuichezea timu hiyo.
