Rosario, Argentina
Supermarket inayomilikiwa na familia ya mke wa mwanasoka, Lionel Messi imevamiwa na majambazi wenye silaha ambao wameacha ujumbe wa kuitishia maisha familia hiyo.
Polisi mjini Rosario nchini Argentina iliyopo Supermarket hiyo wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Alhamisi ambapo milio ya risasi ilisikika mara 14 kwenye mlango wa mbele na kwenye madirisha.
Tukio hilo lilifanywa na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki, na ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa kwa risasi katika Supermarket hiyo ya Unico maarufu kwa kuuza vyakula hofu imekuwa kubwa.
Polisi pia walisema kwamba wavamizi hao baada ya kufyatua risasi waliacha taarifa iliyoandikwa kwenye ubao na kusomeka, “Messi tunakusubiri wewe, Javkin anajihusisha na madawa ya kulevya, hawezi kuwa makini na wewe.”
Uchunguzi unaendelea na Javkin ambaye jina lake ni Pablo Javkin ndiye meya wa mji wa Rosario, mji mkubwa katika jimbo la Santa Fe, kusini mwa mji mkuu wa Buenos Aires nchini Argentina.
Baada ya tukio hilo Javkin alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuzungumzia ongezeko la matukio ya uhalifu na uhaba wa polisi na kutokuwapo ulinzi wa kutosha katika mji huo.
Hii si mara ya kwanza kwa Javkin kutoa malalamiko hayo, mapema wiki hii alizungumzia ukosefu wa ulinzi na umuhimu wa kuwa na polisi wengi katika mji huo ambao uhalifu umekuwa ukiongezeka.
Messi na mkewe Antonela Roccuzo hawajasema lolote kuhusu tukio hilo ambalo limetokea siku takriban siku nne baada ya Messi kutwaa tuzo ya Fifa ya mchezaji bora mwanaume baada ya kuiongoza Argentina kubeba taji la dunia Desemba mwaka jana.
Kimataifa Familia ya Messi yatishiwa maisha
Familia ya Messi yatishiwa maisha
Read also
