Paris Ufaransa
Waendesha mashitaka nchini Ufaransa wameanza uchunguzi wa awali wa tuhuma za kubaka zinazomkabili beki wa klabu ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, Achraf Hakimi.
Uchunguzi huo unaendeshwa na ofisi ya waendesha mashtaka wa kitongoji cha Naterre katika jiji la Paris yalipo makao makuu ya klabu ya PSG.
Habari zaidi zinadai kwamba msichana mmoja wa miaka 23 alikwenda polisi mwishoni mwa wiki na kuripoti kuwa Hakimi mwenye umri wa miaka 24 alimbaka.
Msichana huyo hata hivyo hakufungua kesi yoyote dhidi ya Hakimi badala yake alichofanya ni kama kuwasilisha taarifa polisi ingawa ofisi ya waendesha mashitaka iliamua kuanza uchunguzi wa tukio hilo.
Maofisa wa klabu ya PSG hadi sasa bado hawajasema lolote kuhusu kadhia iliyomkumba mchezaji wao na hata mchezaji mwenyewe hajatoka hadharani kukiri au kukanusha tuhuma hizo.
Hakimi ambaye ana asili ya Morocco lakini ni mzaliwa wa Hispania, alikuwa katika kikosi cha timu ya Morocco kilichoweka historia kwenye fainali za Kombe la Dunia Desemba mwaka jana.
Katika mechi ya Jumapili iliyopita ya PSG dhidi ya Marseille, Hakimi hakucheza kwa sababu alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya misuli.
Habari za ndani kutoka PSG zinadai kwamba pamoja na tuhuma hizo mchezaji huyo anaweza kuiwakilisha timu yake keshokutwa Jumamosi katika mechi dhidi ya Nantes.
Kimataifa Beki PSG atuhumiwa kubaka
Beki PSG atuhumiwa kubaka
Read also
