Na mwandishi wetu
Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma au MwanaFA amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuwataka wasanii na wanamichezo kufanya kazi kwa mikono yao.
MwanaFA ambaye ni mwanamuziki mkongwe nchini ni miongoni mwa uteuzi uliotangazwa Jumapili hii na Rais Samia kabla ya kula kiapo Jumatatu akichukua nafasi ya Pauline Gekul aliyehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao kijamii wa Instagram, MwanaFA aliweka ujumbe huo wa shukrani kwa Rais sambamba na kuwasihi wadau wa wizara hiyo kwenda kufanya kazi kwa bidii.
“Wanautamaduni,wasanii na wanamichezo wa nchi hii, muda ndio huu jamaa zangu, twendeni tukafanye mambo yetu kwa mikono yetu wenyewe, Mungu ametoa kibali,” alisema MwanaFA
“Namshukuru sana Rais Samia kwa imani hii kubwa aliyonipa kijana wake, ina maana kubwa mno na naahidi kufanya kila lililo ndani ya uwezo wangu nisimuangushe.
“Nawashukuru pia wananchi wenzangu wa Muheza kwa imani na ushirikiano mkubwa wanaoendelea kunipatia. Muheza ni ya watu magwiji watupu,” aliandika FA.
