London, England
Man United imefuta ukame wa mataji kwa kubeba taji la ligi baada ya kuilaza Newcastle mabao 2-0 lakini bado inataka taji jingine, ni lipi? Ligi Kuu England (EPL), Europa Ligi au FA?
Mara ya mwisho Man United kubeba taji ilikuwa msimu wa 2016-17 wakati huo ikiwa chini ya Jose Mourinho na sasa kiungo wa timu hiyo, Bruno Fernandes anasema taji hilo halitoshi wanataka jingine.
“Tumekuwa tukiipigania hatua hii, sasa nimeridhika lakini nataka zaidi, ni taji la kwanza la msimu lakini tunataka zaidi na tunahitaji zaidi, hili halitoshi kwa hii klabu,” alisema Fernando nyota kutoka Ureno.
Kwa Man United kombe hilo ambalo pia linafahamika kama taji la Carabao wanakuwa wamelibeba mara ya sita katika historia ya michuano hiyo wakiwa nyuma ya Liverpool waliolibeba mara nane.
Man United ilineemeka kwa bao lililofungwa na kiungo wa timu hiyo, Mbrazil Casemiro pamoja na bao la kujifunga lililotokana na makosa ya beki wa Newcastle, Sven Botman.
Wakiwa chini ya Mourinho, Man United walibeba taji hilo pamoja na lile la Europa Ligi kabla ya kocha huyo ambaye pia aliwahi kuzinoa klabu za Chelsea, Inter Milan na Real Madrid kutimuliwa.
Mbio za klabu hiyo hazijaishia kwenye taji la ligi, bado wanakimbizana kuwania mataji ya ndani England na Ulaya wakiwa tayari wamewatoa Barcelona au Barca katika Europa Ligi na kufuzu hatua ya 16 bora.
Jumatano hii Man United watakuwa uwanjani kuikabili West Ham katika mechi ya Kombe la FA raundi ya nane hapo hapo wanashika nafasi ya tatu EPL nyuma ya vinara Arsenal kwa tofauti ya pointi nane.

Zimebaki mechi 14 kabla ya msimu wa EPL wa 2022-23 kufikia tamati, hiyo maana yake ni kwamba taji hilo bado liko wazi kwa timu yoyote kulibeba kama ilivyo kwa taji la FA na Europa Ligi.
Kauli ya Fernandes pia iliungwa mkono na kocha wa timu hiyo, Eric ten Hag aliyesema anachotaka sasa ni kushinda tu hasa baada ya kuwekeza tangu mwanzo kuanzia kwa maofisa wa timu.
“Nataka kushinda, tumewekeza tangu mwanzo kuanzia maofisa wanaofanya kazi nzuri pamoja na wachezaji, wote wana hasira na shauku ya kushinda mataji, Man United ipo kwa ajili ya mataji,” alisema Ten Hag.
