Manchester, England
Ushindi wa mabao 2-1 ambao Man United imeupata jana Alhamisi usiku dhidi ya Barca, umempa jeuri kocha wa timu hiyo Erik ten Hag ambaye amesema sasa wanaweza kuifunga timu yoyote.
Man United ikiwa nyumbani Old Trafford iliibuka na ushindi huo katika mechi ya Europa Ligi na sasa inajiandaa kucheza hatua nyingine ya michuano hiyo huku ikiwa imeitoa Barca katika mashindano hayo.
Ushindi huo ni tukio jingine kubwa la timu hiyo kuwaangusha baadhi ya vigogo wa soka barani Ulaya msimu huu ikiwa tayari imeshazipa vipigo, Arsenal na Liverpool za England.
Ten Hag katika kudhihirisha anavyojiamini alisema kwamba kuanzia sasa hadi mwezi Mei hawatoiogopa timu yoyote, “Unahitaji matokeo mazuri ili uamini una nguvu,” alisema kocha huyo Mholanzi.
“Nafikiri hii ni hatua nyingine muhimu kwani unapoifunga Barcelona (Barca), moja ya timu bora katika hatua hii ya Ulaya, hapo unakuwa unajiamini kwamba uko imara na kuwa tayari kumfunga yeyote.”
“Ulikuwa ni usiku wa kipekee, nafikiri ni jambo ‘bab kubwa’ unapoifunga Barcelona, inaongoza La Liga ikiwa mbele ya Real Madrid kwa pointi nane na tumeona Real ilivyocheza wiki hii (imeifunga Liverpool 5-2),” alisema Ten Hag ambaye huu ni msimu wake wa kwanza Man United.
“Tumecheza katika kiwango kizuri na tunatakiwa kuendelea hivyo msimu huu, kuendelea na kiwango hiki katika kuamini kwamba tunaweza kushinda mechi kubwa,” alisema.
Katika mechi hiyo, Barca ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 18 lililofungwa na Robert Lowandowski kwa penalti iliyotolewa baada ya Bruno Fernandes kumchezea rafu Alejandro Balde.
Man United iliandika bao la kusawazisha dakika ya 47 lililofungwa na Fred kabla Mbrazil mwenzake Antony hajamalizia bao la pili dakika ya 72.
Katika mechi ya awali baina ya timu hizo iliyopigwa Nou Camp, matokeo yalikua sare ya mabao 2-2 na hiyo maana yake ni kwamba Man United sasa inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.
Matokeo mechi za Europa Ligi Alhamisi hii…
Nantes 0-3 Juventus
PSV Eindhoven 2-0 Sevilla
Man Utd 2-1 Barcelona
FC Midtjylland 0-4 Sporting
Monaco 2-3 B Leverkusen
(B Leverkusen 5-3 Monaco-penalti)
Union Berlin 3-1 Ajax
Rennes 2-1 Shakhtar Donetsk
(Shakhtar Donetsk 5-4 Rennes-penalti)
Roma 2-0 RB Salzburg
