Barcelona, Hispania
Baada ya habari za Lionel Messi kutaka kurejea Barcelona kuibuka kwa mara nyingine, kocha wa timu hiyo, Xavi Hernandez amesema wakati wote milango itakuwa wazi kwa mchezaji huyo kurejea.
Habari hizo zinachangiwa na ukweli kwamba mchezaji huyo aliyejipatia umaarufu wakati akiichezea Barca, atamaliza mkataba wake na PSG mwishoni mwa msimu huu na hivyo lolote linaweza kutokea.
Wakati habari za Messi zikiibuka na kuzama kabla ya kuanza msimu huu, safari hii inadaiwa baba wa mchezaji huyo, Jorge amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Barca, Joan Laporta hivi karibuni.
Katika kikao hicho inadaiwa suala la Messi lilijadiliwa ikiwa ni mara ya kwanza tangu mchezaji huyo aihame Barca mwaka 2021 na kujiunga na vigogo hao wa jiji la Paris.
“Hapa ni nyumbani kwake na mlango wakati wote utakuwa wazi,” alisema Xavi ambaye leo usiku timu yake itaumana na Man United katika mechi ya Europa Ligi hatua ya 16 bora.
“Messi ni rafiki na wakati wote tunawasiliana, inategemea nini anakihitaji kwa siku zijazo na namna klabu itakavyolichukulia suala hilo, ni mchezaji bora duniani na anaendelea kuwa hivyo, wakati wote anafa kwenye timu,” alisema Xavi.
Habari za ndani zinadai kwamba PSG nao bado wana nia ya kumuongezea mkataba Mess ambaye pia amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na klabu ya Miami FC ya Marekani pamoja na klabu kadhaa za Saudi Arabia.
