Na mwandishi wetu
Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) limeomba kurudishwa kwa mchezo wa mpira wa kikapu katika mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta).
Michael Mwita ambaye ni Katibu Mkuu wa TBF alifafanua kuwa kwa muda sasa mchezo huo umekuwa ukihusishwa kwenye michuano ya shule za sekondari lakini imekuwa tofauti kwenye mashindano ya shule za msingi.
Alifafanua kuwa lengo la shirikisho hiloni kuhakikisha mchezo huo unachezwa hasa na rika la watoto wadogo kuanzia angalau miaka minane maana ndio umri sahihi wa kumjenga mtoto katika mchezo huo.
“Takriban miaka kumi au zaidi sasa mchezo huu umekuwa haushirikishwi au umetolewa katika orodha ya michezo ambayo ipo katika mashindano ya Umitashumta kwa kushirikiana na mikoa na wadau wa maendeleo ya mchezo tumefikiri na kuona upo uwezekano wa kuwepo tena katika mashindano hayo kutokana na vigezo ambavyo tutaviainisha.
“Msingi wowote wa maendeleo huanza kuandaliwa akiwa mtoto, ndipo anapofundishwa kuwa bora zaidi hata timu za Taifa zinapatikana kupitia maandalizi ya timu za watoto, kikapu kwa sasa unakua kwa kasi na unalipa,” alisema Mwita.
