Na mwandishi wetu
Kipa wa Yanga, Abuutwalib Mshery atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu akiuguza goti baada ya kufanyiwa upasuaji hivi karibuni.
Mshery ambaye kwa muda mrefu amekuwa nje ya uwanja kutokana na majeraha hayo amerejea hivi karibuni akitokea Tunisia alikokwenda kufanyiwa matibabu.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe ameiambia GreenSports kuwa kipa huyo hatakuwepo kwenye kikosi hicho kwa miezi kuanzia mitatu hivyo itamlazimu kukaa nje hadi mwisho wa msimu kutokana na muda uliobaki kabla ya ligi kumalizika.
“Mshery anaendelea vizuri, amefanyiwa upasuaji na matibabu yaliyotakiwa na sasa atakuwa nje ya uwanja kuanzia miezi mitatu kulingana na jeraha alilokuwa nalo na muda atakaotumia kupona na kurejea katika kikosi,” alisema Kamwe.
Hata hivyo, mapema kabla ya kumfanyia upasuaji huo, Yanga ilishamsajili Metacha Mnata kutoka Geita Gold kwenye usajili wa dirisha dogo hivi karibuni ili kuziba nafasi ya Mshery aliyetua Yanga msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
