Chartlotte, Marekani
Leo, Ijumaa Februari 17, nyota wa zamani wa mpira wa kikapu, Michael Jordan anasherehekea miaka 60 ya kuzaliwa kwa kutoa dola 10 milioni (zaidi ya Sh 23 bilioni za Kitanzania) ili kusaidia jamii.
Jordan, bingwa mara sita wa NBA, ametoa misaada hiyo kwa taasisi ya Make-A-Wish ikiwa ni kiasi kikubwa zaidi cha fedha kuwahi kutolewa na mtu mmoja katika miaka 43 ya historia ya taasisi hiyo.
Akizungumzia uamuzi huo, Jordan alisema kwamba anaamini hatua yake ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kutoa msaada wa aina hiyo itawahamasisha watu wengine kufanya hivyo ili kuipa nguvu taasisi hiyo ambayo husaidia watoto wenye shida mbalimbali.
“Kwa miaka 34 iliyopita imekuwa heshima kwangu kushirikiana na Make-A-Wish na kusaidia kuwapa tabasamu na furaha watoto wengi,” alisema Jordan katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Jordan ambaye kwa sasa anamiliki timu ya mpira wa kikapu ya NBA ya Charlotte Hornets, kwa mara ya kwanza alianza kuisaidia taasisi ya Make-A-Wish mwaka 1989.
Mwaka 2008, alitangazwa kuwa balozi wa Make-A-Wish kwa kile ambacho taasisi hiyo ilikitaja kuwa ni mchango wake ulivyokuwa na maana katika kuhakikisha matarajio ya watoto na familia zao yanatimia.
“Siwezi kufikiria zawadi bora ya siku ya kuzaliwa zaidi ya kuona watu wanaungana nami katika kuisaidia Make-A-Wish ili kila mmoja aweze kushuhudia maajabu ya kufanya matamanio ya watoto yatimie,” alisema Jordan.
