London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amemshutumu ofisa Lee Mason akidai hajui kazi yake katika kufuatilia picha za VAR na sasa timu yake ina kazi ya kupigania pointi mbili ilizopoteza katika mechi na Brentford.
Jumamosi iliyopita, Arsenal ilitoka sare ya 1-1 na Brentford katika Ligi Kuu England (EPL), ikiumizwa na bao la dakika ya 74 lililofungwa kwa kichwa na Ivan Toney licha ya mtoaji pasi Christian Norgaard kutoa pasi hiyo akiwa eneo la kuotea.
Baada ya kubaini ofisa huyo alifanya kosa, Bodi ya Wataalam Wasimamizi wa Mechi (PGMOL) ilitoa taarifa ikidai ni kosa la kibinadamu ingawa Mason alisimamishwa kazi na Arsenal kuombwa radhi.
Arteta ambaye timu yake inashika usukani katika EPL licha ya kuombwa radhi bado alililalamikia tukio zima ambalo alidai liliwaneemesha wapinzani wao Man City ambao leo Jumatano usiku wanaumana katika mechi ya EPL inayotarajiwa kuwa ngumu.
Arsenal inaongoza ligi ikiwa na pointi 51 ikifuatiwa na Man City yenye pointi 48 na kama si tukio la mechi ya Brentford, Arteta anaamini wangeizidi Man City kwa pointi tano na si tatu za sasa ingawa Arsenal imecheza mechi 21 hadi sasa na Man City 22.
Kocha huyo alisema kwamba wamesikitishwa na tukio hilo na kusisitiza kwamba halikuwa kosa la kibinadamu badala yake ni mtu kutoijua kazi yake jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.
“Ni tukio ambalo limeinyima Arsenal pointi mbili ambazo hatuwezi kurudishiwa, tutakwenda kuzitafuta pointi hizo kwingineko kwenye ligi,” alisema Arteta.
“Wakati huo huo tunashukuru kwa kuombwa radhi na taarifa iliyotolewa, wenzetu wengi wengine katika soka wametupa pole na kusema kwamba wasingeweza kucheza soka kwa heshima kama tulivyofanya sisi, hiyo ndiyo hali halisi ni lazima tuangalie mbele,” alisema Arteta.
“Tukio hili limewafanya wachezaji, maofisa wa timu na mashabiki kuwa imara zaidi na kuwaongezea shauku ya kukipita kipindi hiki kigumu na kutupa sisi jukumu hilo, na kwa hilo tupo tayari,” alisema.
Alipoulizwa iwapo ameridhishwa na maelezo ya PGMOL, Arteta alisema, “Nitaridhika tu kama wataturudishia pointi mbili jambo ambalo haliwezekani.”
“Nashukuru na nafikiri walikuwa waungwana, wawazi na wakweli kwa kuomba msamaha na kutoa taarifa, ni jambo zuri lakini haliondoi ukweli kwamba tuna pungufu ya pointi mbili ambazo tulitakiwa kuwa nazo kwenye msimamo wa ligi,” alisema.
Kiongozi mkuu wa PGMOL, Howard Webb ambaye ni mwamuzi wa zamani aliwasiliana na Arsenal na kuwaelezea tukio zima ikiwamo kuomba radhi kabla ya kuitisha kikao na waamuzi wa EPL jana Jumanne.
Katika kikao hicho inaaminika ilielezwa kuwa walijadiliana matumizi ya VAR baada ya kuibuka malalamiko mengi katika siku za hivi karibuni licha ya matarajio ya awali kuwa VAR ingekuwa mwarobaini wa makosa katika mechi za soka.
