Na mwandishi wetu
Wakati Simba ikijipanga kwa mechi yao ya wikiendi hii dhidi ya Raja Casablanca imeeleza kurejea kwa kiungo mshambuliaji wao, Saido Ntibazonkiza ambaye alikosekana kwenye mechi iliyopita.
Saido hakuwepo kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya AC akielezwa ni majeruhi. Katika mechi hiyo, Simba ilifungwa bao 1-0.
Akizungumza Jumanne hii jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema mchezaji ameshatengemaa, amepumzika kama ilivyotakiwa na sasa atajiunga na kambi ya timu hiyo kuelekea mechi ijayo akiwa fiti.
“Saido ambaye hatukusafiri naye Guinea alikuwa na majeraha kama tulivyoeleza, akapewa muda wa kupumzika, kupata matibabu pia lakini sasa ametengemaa na timu itakaporejea kambini naye atarejea, hii ni kusema kwamba atakuwa sehemu ya mchezo,” alisema Ally.
Ofisa huyo pia aligusia kurejea kwa majeruhi mwingine, Peter Banda ambaye atajiunga na kambi kisha atafanyiwa vipimo ili madaktari wajiridhishe kama atakuwa sehemu ya mchezo au la.
Pia alitolea ufafanuzi kukosekana kwa kiungo wa kati, Sadio Kanoute ambaye ataukosa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
“Sadio alioneshwa kadi ya njano kwenye mchezo wetu na Horoya, sasa tunathibitisha kwamba Kanoute ataukosa mchezo kutokana na kadi tatu za njano. Kikanuni kadi alizopata hatua ya awali anaondoka nazo hadi hatua ya makundi, ndiyo maana kadi aliyopata majuzi inamfanya aukose mchezo ujao,” alisema.
Katika hatua nyingine, Ally alitangaza kushuka kwa bei za viingilio vya mchezo huo ambapo viti vya mzunguko vilivyokuwa Sh 5,000 sasa ni Sh 3,000, VIP C imeshuka kutoka Sh 20,000 hadi Sh 10,000 huku VIP B ikisalia Sh 20,000 na VIP A ni Sh 30,000.
Pia, Ally alitangaza kauli mbiu yao kuelekea mchezo huo dhidi ya Wamorocco hao ni Moto ni Ule Ule, kwa Mkapa hatoki mtu, akidai moto ulioziunguza timu nyingine za Kaskazini mwa Afrika kwenye Uwanja wa Mkapa zilipokuja kucheza na Simba, ndiyo utakaowaangamiza wapinzani wao hao.
